Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaelekeza anayedai mil 139/- aombe kukamata mali

506bef7276711c36f10f9afcae640f3b Mahakama yaelekeza anayedai mil 139/- aombe kukamata mali

Thu, 11 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Ardhi imemuelekeza mdai Prosper Rweyendera kubadili maombi ya kutaka kumfunga jela mchungaji Godfrey Mallasy kwa kushindwa kulipa Sh milioni 139 badala yake awasilishe ombi la kukamata mali za mdaiwa.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu divisheni ya Ardhi, Safina Semfukwe alitoa maelekezo hayo jana baada ya mdaiwa Mallasy kushindwa kulipa kiasi hicho cha fedha na kuomba alipe Sh milioni 12.

Rweyendera alipinga ombi la Mallasy na alitaka alipwe kiasi hicho kama ilivyoamriwa na Mahakama. Mchungaji Mallasy alidai kuwa alikutana na wakili wa mdai, Evodius Rutabingwa na kumueleza mpango wake wa kulipa deni hilo.

Alidai kwamba kesi ilikuwa ya Kanisa la City Christian Fellowship lililokuwa Sinza Palestina Dar es Salaam, na kwamba yeye alikuwa kiongozi lakini baada ya mgogoro kumalizika, kanisa lilisambaratika na akabaki yeye.

Mallasy alisema, aliomba mdai amsamehe na alipokataa aliomba amlipe Sh milioni 12 na kwamba, kila mwezi angelipa Sh 200,000 kwa sababu hana kipato kwani alikuwa anategemea kanisa ambalo kwa sasa halina waumini.

Kwa mujibu wa mdaiwa hivi sasa anapata fedha anapoitwa kwenda kutoa mada. Wakili wa mdai Rutabingwa alidai ni kweli mdaiwa aliomba kupunguziwa deni kutoka Sh milioni 139 hadi Sh milioni 12.

Alidai kwa mazingira ya kesi mteja wake alikataa na kuomba alipwe kiasi hicho kama ilivyoamriwa na Mahakama na akishindwa wanaomba amri ya kumpeleka gerezani.

Baada ya maelezo hayo, Semfukwe alisema "nawashauri mfanye marekebisho ya maombi yenu ya kumpeleka gerezani kwani magereza yetu kwa wahalifu wetu hayatoshi hata kama mteja ana uwezo wa kulipa gharama za kuishi huko kama kuna mali mfanye marekebisho na ombi la kwanza liwe kukamata mali."

Alisema suala la kwenda gerezani hufanyika endapo mdaiwa hana mali hata hivyo, mdaiwa alidai ana nyumba lakini ni ya familia.

Baada ya kueleza hayo, Semfukwe alimtaka mdaiwa kuangalia anafanyaje ili kulipa hilo deni kwa kuwa kesi ipo kwa jina lake.

Aliwataka wadai wafanye marekebisho ambayo wataambatanisha nyumba ya mchungaji huyo ili ikamatwe kwa ajili ya kulipa deni hilo.

"Wakati hawa wanaendelea kuwasilisha maombi, wewe uangalie namna ya kulipa deni kabla amri ya kukamata nyumba haijatolewa," alisema Semfukwe.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 12 mwaka huu. Katika kesi hiyo, Aprili 2016 Mahakama hiyo iliamuru kanisa hilo liondolewe mara moja na kumuachia mdai eneo.

Uamuzi ambao ulitolewa na Jaji John Mgeta na hukumu ilisomwa na Msajili wa Mahakama, Richard Kabate.

Mdaiwa aliamuriwa kulipa kodi ya Sh milioni moja kila mwezi tangu walipoacha kulipa mwaka 2004.

Chanzo: www.habarileo.co.tz