Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaamuru raia wa kigeni anayedaiwa kusimika mitambo ya mawasiliano kukamatwa

67417 Mahakama+pic

Thu, 18 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kukamatwa raia wa Moldovan, Vadim Burin anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kusimika mitambo ya mawasiliano ya simu za kimataifa bila leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kuisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya Sh41.7 milioni.

Mbali na Burini, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ni dereva taksi, Msafiri Msayi mkazi wa Kivule.

Burini na Msanyi wanakabiliwa na mashtaka nane, yakiwemo ya kuingiza nchini vifaa vya mawasiliano na kutumia simu 210 ambazo hazijasajiliwa.

Hata hivyo, Msanyi amesomewa mashtaka yake leo Alhamisi Julai 18, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Salum Ally.

Akimsomea hati ya mashtaka wakili wa Serikali Mkuu, Monika Mbogo, akisaidiana na wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon na Batilda Mushi amedai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka nane.

Mushi amedai kuwa katika shtaka la kwanza siku na mahali tofauti jijini Dar es Salaam walikula njama kutumia mtandao isivyo halali.

Pia Soma

Katika shtaka la pili, imedaiwa Mei 15, 2019 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) washtakiwa kwa pamoja waliingiza nchini vifaa vya elektroniki vya mawasiliano  bila leseni kutoka TCRA.

Shtaka la tatu, washtakiwa wanadaiwa kusimika mifumo ya elektroniki bila leseni ya TCRA.

Katika shtaka la nne, Simon amedai kati ya Mei 15 na Juni 10, 2019  katika eneo la Hotel ya SeaCliff walitumia vifaa vya mawasiliano kwa lengo la kupokea na kutoa mawasiliano bila kuwa na kibali cha TCRA.

Pia inadaiwa Mei 15, 2019 katika eneo la Hoteli ya Sea Cliff iliyopo Masaki, washtakiwa waliendesha mtandao wa mawasiliano ya kimataifa bila leseni ya TRCA.

Simon amedai  shtaka la sita katika Hoteli ya Sea Cliff washtakiwa walitumia laini za simu 173 za mtandao wa Halotel na 37 za mtandao wa Vodacom ambazo hazijasajiliwa huku wakijua ni kinyume cha sheria.

Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa  katika shtaka la nane, washtakiwa wote wanadaiwa  kuisababishia  Serikali na TCRA hasara ya Sh 41,710,800.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Wakili Mbogo aliiomba mahakama kutoa hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa wa kwanza Burin ili aweze kuunganishwa katika kesi hiyo.

Hakimu Ally amesema mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote.

"Mahakama inatoa hati ya kumkamata Burin na mshtakiwa wa pili katika kesi hii apelekwe mahabusu na  Agosti Mosi, 2019 kesi hii itakapotajwa,” amesema Hakimu Ally.

Chanzo: mwananchi.co.tz