Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, Harbinder Seth na mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege wapelekwe katika mahakama hiyo kwa kuwa gereza la Ukonga halina huduma ya kuendesha kesi kwa njia ya mtandao.
Mbali na washtakiwa hao mwingine ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL, James Rugemarila wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi yakiwemo mashtaka matano ya kutakatisha fedha na kuisababisha hasara.
Hatua hiyo imekuja leo Alhamisi Aprili 9, 2020 baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon kudai kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa hao hawapo katika mahakamani hiyo kutokana na mshtakiwa Seth na Makandege kuwapo katika gereza la Ukonga ambalo halina huduma ya kuendesha kesi kwa njia ya mtandao. "Mheshimiwa tumeendesha shauri hili bila ya washtakiwa kutokuwepo mahakamani Rugemarila yupo katika gereza la Segerea ambapo huduma ya kuendesha kesi kwa njia ya mtandao ipo lakini Seth na Makandege wapo Ukonga huduma hiyo haipo hivyo naiomba mahakama hii ihairishe tarehe nyingine,"alieleza Simon.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema kutokana gereza la Ukonga kutokuwa na huduma ya kuendesha kesi kwa njia ya mtandao hivyo ameamuru mshtakiwa Seth na Makandege waletwe katika mahakama hiyo wakati shauri hilo litakapokuja kwa ajili ya kutajwa huku mshtakiwa Rugemarila atasikiliza kwa kupitia njia ya mtandao akiwa katika gereza la Segerea.
Kesi hiyo imeahirishwa ha Aprili 23, 2020 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.