Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yaagiza hati ya mashtaka kesi ya Mbowe, vigogo Chadema kurekebishwa

8824 Kesi+pic.png TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeuamuru upande wa mashtaka kufanya marekebisho katika hati ya mashtaka yanayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na vigogo wengine nane wa chama hicho.

Uamuzi huo umetolewa  leo Jumatatu Juni 11, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu,  Wilbard Mashauri.

Baada ya kutoa uamuzi huo, wakili wa utetezi Peter Kibatala alieleza mahakamani hapo kuwa hawajaridhishwa na uamuzi huo  na akawasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Hakimu Mashauri alitoa uamuzi huo baada ya kupitia mapingamizi nane yaliyowasi?ishwa mahakamani hapo na Kibatala na Jeremiah Mtobesya.

Kwa pamoja, mawakili hao wa upande wa utetezi walikuwa wakiomba mashtaka yanayowakabili  washtakiwa hao yafutwe kwa sababu yana upungufu wa kisheria, ikiwamo shtaka moja kuwa na makosa mawili hoja ambayo ilipingwa na upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo, Hakimu Mashauri  alikubaliana na baadhi ya hoja za upande wa utetezi kuwa  katika shtaka la pili, tatu, nne, tano, sita na saba yana upungufu wa kisheria  na kuamuru upande wa mashtaka kufanya mabadiliko katika hati ya mashtaka.

Baada ya kutoa uamuzi huo, wakili Kibatala aliieleza mahakama kuwa hawajaridhishwa na uamuzi huo hivyo aliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Soma Zaidi: Mbowe ‘atokezea kivingine’ Kisutu

Kibatala amedai kuwa wanakata rufaa kwa sababu wao waliomba mashtaka hayo yafutwe lakini mahakama imeamua yafanyiwe marekebisho kwenye hati ya mashtaka.

Baada ya Kibatala kueleza hayo, wakili wa serikali,  Paul Kadushi amedai kuwa huo ni uamuzi mdogo ambao hauwezi kumaliza kesi na kwamba uamuzi huo hawawezi kuukatia rufaa.Kibatala amesisitiza kuwa kwa kuwa mahakama imeona mashtaka hayo ni batili,

mashtaka hayo yanakufa ndio maana mahakama ikaamuru marekebisho, hivyo watakata rufaa. 

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho hakimu atakapotoa uamuzi kama anaridhika na ombi la upande wa utetezi ama la.

Mbali na  Mbowe wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo namba  112 ya 2018 ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu makatibu wakuu Salum Malimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).

Wengine ni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Kawe, Halima Mdee na mbunge wa Bundam Ester Bulaya.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria na kuendelea kufanya mikusanyiko usio halali ama maandamano yaliyosababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz