Takribani wanafunzi 300 wa shule ya sheria Tanzania wamejengewa uwezo kuhusu utendaji kazi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), hatua itakayowasaidia kuwa na ujuzi wakati wa utelelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Jumamosi Novemba 13, 2021 yakifunguliwa na Rais wa AfCHPR, Jaji Imani Aboud amesema wameamua kutoa mafunzo hayo ili kuwapa uzoefu wanafunzi hao ambao baadhi watakuwa wanasheria watarajiwa katika taasisi mbalimbali pindi watakapohitimu masomo yao.
Jaji Aboud amesema mahakama hiyo inawaelimisha wanafunzi hao masuala mbalimbali tangu ilivyoanzishwa na kwa nini nchi za Afrika takribani 55 zinachangia fedha zake ili kuiendesha.
" Tunataka wanafunzi hawa atambue mahakama hii inatumia sheria na taratibu gani ili wakimaliza chuo wawe na uzoefu na elimu ya kutosha kuhusu mhimili huu. Baadaye watakuwa mawakili wazuri wenye elimu na ufahamu wa masuala ya haki za binadamu," amesema Jaji Aboud.
Mkuu wa Shule ya Sheria ya Tanzania, Benhaji Masoud amesema mafunzo hayo yatawasaidia wanafunzi hao na kusisitiza kuwa masomo wanayoyasoma chuoni hapo kwa vitendo mojawapo ni kuhusu haki za binadamu na uwepo wa mahakama za kimataifa za haki za binadamu.
Akizungumza kwa niaba yake wenzake, mwanafunzi wa shule hiyo, Antony Colyuas amesema mafunzo hayo ni fursa nzuri kwao kwa sababu wamepata sehemu ya kujifunza kwa vitendo kutokana na kile wanachofundishwa darasani.