Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama ya Rufani yaridhia kunyongwa aliyemuua mkwewe

57105 Pic+mahak

Mon, 13 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imepigilia msumari wa mwisho katika adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa mfungwa Mathias Tangawizi, aliyehukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua mama mkwe wake, Sophia Kamuli.

Mathias alihukumiwa adhabu hiyo na Jaji Lameck Mlacha, Machi 14, 2016 baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya jinai namba 65 ya mwaka 2010 kuwa umethibitisha mashtaka dhidi yake bila kuacha shaka yoyote.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi wake, Mathias alimuua mama mkwe wake huyo kwa kumchomachoma kwa mkuki sehemu mbalimbali za mwili wake Mei 24, 2008, akimtuhumu kuwa ni mchawi aliyesababisha kifo cha mtoto wake na kumroga yeye mwenyewe.

Wakati wa utetezi wake alikiri kumuua mama mkwe wake huyo lakini alikana kuwa hakuwa amekusudia kufanya hivyo. Mahakama Kuu haikukubaliana na utetezi wake hivyo ilimtia hatiani na kumhukumu adhabu hiyo.

Hata hivyo alikata rufaa akipinga kutiwa hatiani kwa kosa la kuua badala yake pamoja na mambo mengine akaiomba mahakama imtie hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Alikuwa akidai kuwa alitenda kosa hilo kwa kuamini kuwa mama mkwe wake huyo alikuwa mchawi aliyesababisha kifo cha mwanaye na pia aliyemwekea sumu kwenye chakula.

Pia Soma

Hata hivyo Mahakama ya Rufani katika hukumu yake ilitupilia mbali hoja zote za mrufani alizozitoa wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo kupitia kwa wakili wake Constantine Mutalemwa, badala yake ikakubaliana na hoja za mawakili wa Serikali.

Mahakama hiyo katika hukumu hiyo iliyoandaliwa na Jaji Mwanaisha Kwariko kwa niaba ya majaji wenzake wawili, Mbarouk Mbarouk (kiongozi wa jopo) na Jacobs Mwambegele imesema kwamba madai ya mrufani kutenda kosa hilo kwa imani za kichawi hayana msingi kwani hayakuthibitika.

Ikirejea utetezi wake katika kesi ya msingi, mahakama hiyo imesema kuwa mbali na tuhuma za maneno matupu, mrufani hakuweza kuthibitisha uchawi wowote wa marehemu wa mama mkwe wake.

Imesema mrufani katika ushahidi wake alisema hakuna hata mganga wa jadi kati ya wale waliokwenda kwao kupata matibabu ambaye alimweleza kuwa marehemu alikuwa mchawi na kwamba yeye ndiye aliyemwekea sumu kwenye chakula alichokula.

Mahakama hiyo imebainisha kuwa mrufani alieleza kuwa chakula kinachodaiwa kuwekwa sumu alichoandaliwa na marehemu alipomtembelea nyumbani kwake Septemba 2007 hakikuwa cha kwanza kuandaliwa naye.

Hivyo mahakama ilisema kuwa madai ya mrufani ya kutenda kosa hilo kwa imani za kiuchawi hayakuthibitika na badala yake ilisema kuwa mrufani alikuwa amejenga dhamira ya kumuua mkwewe huyo dhamira ambayo aliitekeleza Mei 24, 2008.

“Hivyo mahakama iliyosikiliza kesi ya msingi ilimtia hatiani kwa usahihi kwa kosa la mauaji na ilimpa adhabu hiyo kisheria. Hoja hii ya rufani haina mashiko,”inasomeka sehemu ya hukumu hiyo na kusisitiza:

“Mwishowe hatuoni sababu ya kukosoa uamuzi wa mahakama iliyosikiliza kesi ya msingi na tunakubali kwamba rufaa hii haina mashiko na tunaifutilia mbali yote.”

Chanzo: mwananchi.co.tz