Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama ya Rufani yaendesha kesi nane kiteknolojia

Mahakama ya Rufani yaendesha kesi nane kiteknolojia

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imeendesha kesi nane kwa njia ya teknolojia ya mawasiliano ijulikanayo kama video conference.

Kesi hizo zimeendeshwa na majaji watatu tofauti jana na leo Jumanne Machi 12, 2019 katika Kituo cha Mafunzo na Habari cha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), kilichopo nyuma ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Kwa kutumia teknolojia hiyo, majaji hao wamefanikiwa kuendesha kesi hizo wakiwa jijini Dar es Salaam huku wadaiwa wakiwa jijini Mbeya, lakini wote wakisikilizana na kuona kwa njia hiyo.

Majaji waliohusika kuendesha kesi hizo kwa nyakati tofauti ni Rehema Mkuye na Sivangilwa Mwangesi ambao wote walisikiliza kesi mbili kila mmoja.

Wengine ni Jaji Dk. Gerald Ndika na Jaji Jacobs Mwambegele ambao pia wamesikiliza kesi mbili kila mmoja.

Akizungumzia teknolojia hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu amesema inarahisisha kazi na pia inapunguza gharama za uendeshaji wa kesi na kuokoa muda.

"Kwa kutumia teknolojia hii hapa kituoni kwa siku moja tunatumia Sh70,000 tu kwa kila kituo hiki na kule Mbeya," amesema Mkwizu akimaanisha kwa vituo viwili kwa siku ni Sh140,000.

"Kwa Court of Appeal (Mahakama ya Rufani) lazima majaji wangu waondoke waende. Wataondoka wao, ataondoka msajili, wataondoka madereva na magari, wanaenda kulala hotelini, watakula unaona hizo gharama zote ambazo tumeziokoa."

Mkwizu amesema kesi zote ilizosikilizwa zilikuwa ni za Mbeya na Sumbawanga na kwamba, kwa ratiba ya mahakama hiyo ilikuwa majaji waende kuwasikiliza wadaiwa huko mwezi Juni, lakini wameweza kuzisikiliza leo kwa urahisi na haraka.

"Kwa hiyo hii system inatusaidia kutimiza vision (mwelekeo) ya mahakama ya utoaji haki kwa wote na kwa wakati," amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz