Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama ya Rufani yaamuru Sheikh Ponda kuhukumiwa upya

65582 Ponda+pic

Fri, 5 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani nchini Tanzania imetengua mwenendo wa hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  iliyomhukumu Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda adhabu ya kifungo cha nje, kutokana na kasoro za kisheria.

Badala yake mahakama hiyo imeamuru Sheikh Ponda arudishwe kizimbani katika mahakama hiyo ya Kisutu, ili kesi iliyokuwa ikimkabili yeye na wenzake 49 ianze upya kuanzia pale alipohukumiwa adhabu hiyo, kusisitiza kufuatwa kwa misingi na matakwa ya kisheria.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Julai 4, 2019 na jopo la majaji watatu; Stella Mugasha (kiongozi ), Ferdnand Wambali na Rehema Sameji baada ya kukubaliana na maombi na hoja za Serikali kuhusu kasoro hizo za kisheria.

Kasoro ilizozibainisha Serikali ambazo Mahakama ya Rufani imekubaliana ni kwamba Mahakama ya Kisutu katika hukumu yake ilimhukumu Sheikh Ponda kutumikia adhabu hiyo ya kifungo cha nje mwaka mmoja, bila kumtia kwanza hatiani, kinyume cha matakwa ya sheria.

Mahakama ya Kisutu katika hukumu yake iliyotolewa na Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, Mei 9, 2013  ilimhukumu Sheikh Ponda kifungo cha nje cha mwaka mmoja kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo la ardhi ya kampuni ya Agritanza Ltd lililopo Chang’ombe Markazi.

Hata hivyo,  Sheikh Ponda kupitia kwa wakili wake, Juma Nassoro alikata rufaa Mahakama Kuu akipinga adhabu hiyo na Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Augustine Shangwa, Novemba 27, 2014, ilitengua hukumu ya Kisutu na kumwachia huru.

Pia Soma

Serikali nayo ikakata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu hiyo ya Mahakama Kuu, na siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo ya Serikali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga alieleza mahakama kuwa wamebaini kasoro katika hukumu ya Mahakama ya Kisutu.

Wakili Katuga amesema kuwa wakati wanapitia kumbukumbu za mahakama walibaini kuwa Mahakama ya Kisutu ilimhukumu Sheikh Ponda adhabu hiyo bila kumtia hatiani kwanza, jambo alilosema ni kinyume cha kifungu cha 235 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Wakili Katuga amesema kutokana na hali hiyo hukumu na mwenendo wa Mahakama Kuu iliyomfutia hatia Sheikh Ponda ni batili na kuomba  mahakama hiyo iamuru Sheikh Ponda arudishwe Kisutu ahukumiwe upya adhabu hiyo kwa kumtia kwanza hatiani kabla ya kumsomea adhabu.

Wakili wa Sheikh Ponda, Juma Nassoro alikubaliana na hoja za wakili Katuga kuwa kweli kuna kasoro hiyo ya kisheria katika hukumu hiyo, kwamba mahakama haikumtia hatiani mrufani

Hata hivyo wakili Nassoro alitofautiana na wakili Katuga kuhusu kile ambacho Mahakama ya Rufani inapaswa kukiamua, aliomba mahakama hiyo iitupilie mbali hukumu yote ya Mahakama ya Kisutu na Mahakama Kuu, na kumwachilia huru kabisa Sheikh Ponda.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika hukumu yake iliyosomwa leo na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, imekubaliana na hoja na maombi ya Serikali na imeamuru Sheikh Ponda arudishwe Kisutu ahukumiwe upya kwa mujibu wa sheria kwa kumtia kwanza hatiani.

Katika kesi ya msingi Kisutu, Ponda na wenzake 49 walikuwa wakikabiliwa na mashtaka  ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6 milioni na kuingia kijinai kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali eneo la ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd.

Ponda na mwenzake Mukadamu Swaleh kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na shtaka jingine zaidi, la uchochezi, lakini wenzake wengine wote waliachiwa huru na Sheikh Ponda pekee ndio akahukumiwa adhabu hiyo.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz