Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama ya EACJ yakataa maombi ya wanavijiji

Wed, 6 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Wakili wa kujitegemea ,Donald Deya  anayewakilisha vijijini vinne kwenye halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro katika kesi namba 10 ya mwaka 2017 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Tanzania ameiomba Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) miezi minne kukamilisha utaratibu wa kumleta mtaalamu wa mipaka kutoka nje ya nchi.

Alitoa maombi hayo wakati wa kesi hiyo leo Jumanne Machi 5, 2019 mbele ya jopo la majaji watano likiongozwa na Jaji Kiongozi wa kitengo cha awali, Monica Mugenyi ambaye hata hivyo ameyakataa maombi hayo akisema mahakama inatekeleza majukumu yake katika kipindi maalumu cha muda uliopangwa.

Akiwasilisha hati ya kiapo cha kuomba kuahirishwa kwa kesi hiyo iliyofunguliwa na vijiji vinne ambavyo ni Ololosokwan, Oloirien, Kirtalo na Arashi vikipinga Serikali ya Tanzania kuwahamisha katika vijiji vyao vilivyosajiliwa amesema sababu ya msingi ameshindwa kupata mtaalamu wa mipaka ambaye atabainisha mipaka halisi kati ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vijiji hivyo.

“Tangu tulipokutana Desemba mwaka jana hadi leo nimejitahidi kwa namna nilivyoweza kuwapata wataalamu wa mipaka hapa nchini lakini hawakuwa tayari kujihusisha kwenye kesi ambayo inaihusu serikali hivyo nimeshafanya mawasiliano muhimu ya kuwapata wataalamu hao nje ya nchi,” alisema Deya

Akijibu hoja hizo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Aboubakari Murisha akisaidiwa na mawakili wa Serikali, Pauline Mdendemi na Hosana Mgeni amesema hoja za wakili wa walalamikaji hazina msingi kwa sababu ameshindwa kuwaleta mahakamani mashahidi wawili ambao ni Japhet Reiya na Kutiti Klewa bila sababu za msingi.

Murisha amesema katika hoja za Wakili Deya hakuwataja kwa majina wataalamu hao wa mipaka kwa majina wala nchi wanakotoka hatua aliyoitafsiri kama ucheleweshaji wa kesi hiyo kwa makusudi jambo ambalo aliomba mahakama ilikatae.

“Waheshimiwa majaji upande wa serikali tupo tayari kuendelea na kesi hii na leo hii nimekuja na mashahidi watano wakiwemo maofisa waandamizi wawili (Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro) na (Mkurugenzi Mtedaji wa Halmashauri) ambao mchakato wa kupata vibali vya kuwa nje ya kituo chao unachukua muda na gharama za kifedha,” alisema Mrisha

Jaji Mugenyi akitoa uamuzi wake amesema mahakama imetupilia mbali maombi ya walalamikaji kutumia muda wa miezi minne kumpata mtaalamu wa mipaka na kuhoji kwa nini mashahidi wawili hawakuletwa kutoa ushahidi wao ili kusubiri mtaalamu wa mipaka siku nyingine.

Kesi  hiyo ilifunguliwa na vijiji vinne wakipinga serikali kuchoma maboma yao na kuwahamisha kwa nguvu katika maeneo ya vijiji vyao kwa madai kuwa wapo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kinyume cha sheria jambo ambalo wanalipinga.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni mwaka huu, majaji wengine waliosikiliza shauri hilo ni Dk Faustine Ntezilyalo,Fakihi Jundu,Audace Ngiye na Charles Nyachae.



Chanzo: mwananchi.co.tz