Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama mpya ya udhalilishaji yapokea kesi 160

18e201f7496f3490790712517f5205f2 Mahakama mpya ya udhalilishaji yapokea kesi 160

Sun, 25 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAHAKAMA maalumu kwa ajili ya kusikiliza kesi za vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia iliyoanzishwa hivi karibuni tayari imepokea jumla ya kesi 160 katika kipindi cha miezi mitatu huku kesi mbili zikitolewa hukumu kwa watuhumiwa.

Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Vuga Mohamed Ali Mohamed alisema mahakama hiyo ambayo imeanzishwa kutokana na ushauri wa Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi imepokea kesi hizo ikiwemo za udhalilishaji wa kijinsia ubakaji,ulawiti na makosa mengine ya kukashifu wanawake.

Alisema kuwa kesi mbili zimesikilizwa na kutolewa hukumu ya kifungu kuanzia miaka 15 hadi 18 wakati nyingine zikiendelea kusikilizwa zikisubiri uchunguzi zaidi.

“Mahakama maalumu kwa ajili ya kusikiliza kesi za udhalilishaji wa kijinsia tayari imeanza shughuli zake ambapo tumepokea jumla ya kesi 160...tunaendelea na mwenendo wa kusikiliza keso hizo huku nyengine zikihitaji uchunguzi zaidi,” alisema.

Aidha alisema wanakabiliwa na tatizo la uhaba wa mahakimu ambapo kwa bahati nzuri serikali tayari imetoa kibali cha kuajiri watumishi wapya wa mahakama.

Alisema mchakato umeanza kupitia Tume ya Uajiri wa Mahakama ya Zanzibar kutangaza majina ya watu wenye sifa kwa ajili ya ajira katika mahakama mbali mbali za Unguja na Pemba.

“Tukikamilisha mchakato wa kuajiri mahakimu zaidi matarajio yetu tutasikiliza kesi za udhalilishaji wa kijinsia kwa kasi mpya na ari kama tulivyoagizwa na rais wa Zanzibar kuhakikisha kesi za aina hiyo zinasikilizwa kwa wakati ili kupunguza malalamiko ya jamii,” alisema.

Mapema Mkuu wa Kitengo cha Utafiti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) Ramadhan Abdalla Nasib alisema katika kipindi cha miezi mitatu wamekuwa wakitoa mafunzo kwa watendaji katika ofisi ya mkurugenzi mashtaka juu ya kuendesha na kusimamia kesi katika utaratibu unaokubalika kwa mujibu wa sheria.

Alisema katika mafunzo hayo pia yamewashirikisha watendaji wa jeshi la polisi, katika kitengo cha upelelezi ambao kwa kiasi kikubwa wanahusika katika kusimamia mwenendo wa kesi katika upelelezi kabla ya kuziwasilisha ofisi ya Mashtaka ili zifikishwe mahakamani.

“Mfumo wa mpya wa kuendesha kesi za jinai upelelezi unafanywa na jeshi la polisi na baadaye ya kukamilika unaletwa katika ofisi ya mkurugenzi mashtaka kwa kupitia kitaalamu zaidi na baadaye kufikishwa mahakamani tayari kwa ajili ya kutajwa kesi,” alisema.

Mapema Jaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Omar Othman Makungu aliitaka jamii kubadilika na kuwa tayari kutoa ushirikiano wa ushahidi pamoja na kuacha kusuluhisha kesi hizo kwa njia ya maelewano.

Chanzo: www.habarileo.co.tz