Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama Moshi yatupa pingamizi la wakili kesi ya bilionea Olomi

Wed, 22 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, imetupa pingamizi la kutaka kuondolewa, wakili Engelberth Boniphace ambaye anawatetea, mke na mtoto wa marehemu bilionea  Jubilate Olomi katika kesi ya kugombea usimamizi wa mirathi.

Katika  kesi hiyo, me wa marehemu bilionea Olomi, Zainabu Rashid na mtoto wake Julius Jubilate, wanampinga mdogo wa marehemu, Werandumi Olomi kutaka kuwa msimamizi wa mirathi ambapo maamuzi yake yatatolewa (kesho) Mei 22 mwaka huu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Dk Fauz Twaib akitoa uamuzi huo juzi alisema, wakili Boniphace ana haki ya kisheria kuendelea kumtetea mjane huyo na mtoto na mahakama hiyo haina mamlaka ya kumuondoa.

Wakili wa Werandumi Olomi, Joseph Ngiloi alimuwekea pingamizi wakili huyo, kuendelea kumtetea mjane huyo na mtoto wake kwa maelezo kuwa ni mwanasheria  wa halmashauri ya Hai mkoani Kilimanjaro, hana lesseni ya biashara na anavunja sheria za utumishi wa umma.

Jaji Dk Twaib alisema hoja kuwa Wakili Boniface hatakiwi kutetea wateja binafsi kwa kuwa ni mtumishi wa Serikali haina mashiko kwani, wanasheria wa Serikali wanaweza kutetea katika mambo ambayo Serikali imekuwa na maslahi katika mashauri hayo.

Katika uamuzi huo Jaji huyo, alisema si sahihi kuwa, Wakili Boniface anapoteza muda wa kufanyakazi za Serikali kwa kutetea watu binafsi katika shauri hilo, kwa kuwa anatambuliwa kisheria kama wakili na amefuata taratibu zote za kuwa wakili.

Pia Soma

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi mara baada ya maamuzi hayo, Wakili Ngiloi alisema wanakusudia kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.

"Tayari tumeanza taratibu za kukata rufaa na tutaiwasilisha mahakamani, bado tunaamini Wakili Boniphace hapaswi kuendelea kuwa wakili katika shauri hilo," alisema.

Alisema miongoni mwa hoja ambazo atazikatia rufaa ni kuwa, Sheria ya utumishi wa umma inamzuia mtumishi wa Serikali kufanya kazi sehemu mbili tofauti, kwani Boniphace ni mwajiriwa wa Serikali lakini bado anafanyakazi ya uwakili binafsi.

Ngiloi alisema pia, wakili huyo halipi kodi za Serikali kwa kuwa hana leseni ya biashara na hana mashine ya kielektroniki lakini pia anatumia muda wa Serikali kufanyakazi binafsi.

Marehemu Olomi alifariki Januari 15 mwaka huu na kuacha magari kadhaa ya kifahari, majumba katika miji ya Mererani, Arusha, Moshi, Migodi ya Tanzanite, mashamba na mali nyingine kadhaa maeneo mbali mbali nchini zenye thamani ya mabilioni ya fedha.

Awali mgogoro wa mwili wa bilionea huyo na mali zake pia uliwahi kufikishwa kwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na baada ya kushindwa kuelewana pande zote alishauri mgogoro huo kufikishwa mahakamani ili haki ipatikane.

Katika mgogoro wa awali, Zainabu na watoto wake watatu , walikuwa wakiomba haki ya kumzika bilionea huyo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz