Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama Morogoro yazuia Polisi kuwakamata washtakiwa walioachiwa

11808 Mahakama+pic TanzaniaWeb

Thu, 19 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro imezuia utaratibu wa askari polisi kuwakamata washitakiwa wanaofutiwa kesi wakiwa eneo la Mahakama.

Msimamo huo umetolewa leo Julai 19, 2018 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Elizabeth Nyembele, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Waandishi hao wanaohudhuria semina ya uandishi wa habari za mahakamani mkoani Morogoro, walifika mahakamani hapo kwa ziara ya mafunzo.

Hakimu Nyembele amesema mahakama yake imezuia utaratibu huo akisema ni fedheha na kwamba wakati mwingine kitendo hicho kimekuwa kikisababisha madhara makubwa ikiwemo vifo kwa washtakiwa hao wanaofutiwa kesi.

"Sisi hapa kwa sasa tumezuia hilo, zamani ilikuwa inafanyika hata mbele ya hakimu, achilia mbali hiyo ya watuhumiwa kushikilia bendera, mtuhumiwa mwingine anakuja mpaka kwako anasema mheshimiwa nilinde, nilinde, kidogo ni fedheha," amesema Hakimu Nyembele.

Amesema kuna watu wamefariki kwa sababu hiyohiyo ama kwa kugongwa gari wakati wakikimbia kukwepa kukamatwa au kutokana na furaha, askari aliyeko nje anamkimbiza na hata kumpiga risasi akidhani anatoroka.

"Hata wenyewe tunawapa elimu pia kwamba ukiachiwa usikimbie, kwa sababu anaweza kuwa ameachiwa na hakimu mwingine hata ile furaha anaanza kukimbia, askari mwingine hajui kama yule kaachiwa na anamuona amemtoa magereza hivyo, atamshuti, si anajua katoroka," amesema Hakimu Nyembele

Hakimu huyo amesema tayari wameshaonvea na askari polisi kueleza wasifanye hivyo.

Askari polisi wamekuwa na utaratibu wa kuwakamata washtakiwa wanaofutiwa kesi kutokana na sababu mbalimbali, wangali bado wakiwa eneo la mahakama, jambo ambalo limekuwa likisababisha washtakiwa wengine wanaofutiwa kesi kutimua mbio kutoka mahakamani ili kukwepa kukamatwa na polisi.

Wakakati mwingine kumekuwa na purukushani baina ya washtakiwa hao wanaofutiwa kesi na askari wanapojaribu kuwakamata tena.

Awali, akitoa semina kuhusu usikilizwaji wa mashauri ya jinai na mashauri ya madai, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Hakimu Augustino Rwizile amesema si jambo jema kwa washtakiwa wanaofutiwa kesi kukamatwa tena wakiwa katika eneo la mahakama.

Amesema wakati mwingine washtakiwa hao huwa wanakamatwa na kushtakiwa tena kwa makosa yaleyale ambayo yamefutwa jambo ambalo amesema si sahihi.

"Anapokamatwa anaweza kufunguliwa mashtaka hayohayo kwa hakimu mwingine na wakati mwingine huwa wanatudanganya kuwa ana kesi nyingine. Sasa sisi tunakuwa hatujui hilo labda mpaka mshtakiwa mwenyewe ndo aseme kuwa nimeshafutiwa mashtaka haya mahamaani hapa kwa hakimu fulani," amesema Rwizile na kuongeza:

"Mshitakiwa akikamatwa tena baada ya kesi yake kufutwa, akifikishwa mahakamani tena lazima kesi ianze kusikilizwa na siyo kuanza upelelezi tena."

Chanzo: mwananchi.co.tz