Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama Kuu yatengua uamuzi wake usimamizi mirathi ya bilionea Olomi

44007 Pic+ulomi Mahakama Kuu yatengua uamuzi wake usimamizi mirathi ya bilionea Olomi

Wed, 27 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mahakama Kuu imetengua uamuzi wa kumpa Werandumi Olomi haki ya kusimamia kwa muda mirathi ya bilionea Jubilate Olomi aliyefariki Januari 15.

Jaji wa mahakama hiyo, Patricia Fikirini alitoa uamuzi huo jana akisema kuwa alifanya uamuzi wa awali wa kumpa mdogo huyo wa marehemu usimamizi wa muda baada ya kusikiliza upande mmoja wa waleta maombi katika shauri namba 4/2019.

Jaji Fikirini alisema anasimamisha uamuzi huo wa Februari 19 hadi hapo atakaposikiliza pande zote za mgogoro kutokana na unyeti wa suala hilo.

Alisema amechukua uamuzi huo ili kuzuia migogoro na vurugu mahakamani hasa baada ya shauri hilo kuwa tayari limefikishwa katika mahakama nyingine.

“Naagiza aliyepewa haki ya muda kusimamia mirathi, aache mara moja kutekeleza maombi yake hadi hapo tutakapotoa uamuzi mwingine,” alisema.

Jaji Fikirini alimtaka wakili wa Zainabu Rashid, ambaye anadai kuwa ni mke wa marehemu, na Julius Jubilate (mtoto wa marehemu, Engelberth Boniphace kumpa pingamizi lao, wakili wa waleta maombi, Joseph Ngiloi.

Alisema Wakili Ngiloi atajibu pingamizi hilo na kuliwasilisha mahakamani Machi 5, na pande zote zitasikilizwa Machi 6 katika mahakama hiyo.

Akizungumza baada ya uamuzi huo, Wakili Ngiloi alisema watajibu pingamizi hilo kwa wakati na kama ilivyoagizwa na Jaji Fikirini.

“Hatuna tatizo na uamuzi. Sisi tuliomba usimamizi wa muda wa mirathi wakati shauri la msingi likiendelea ili kuweza kupata fedha za kulipa wafanyakazi wa migodi ya marehemu, kulipa gharama za matibabu na ada za shule za watoto wa marehemu,” alisema.

Katika maombi ya Zainabu na mtoto wake Julius, yaliyowakilishwa na Wakili Boniphace, wanaiomba mahakama kuwapa haki ya kusikiliza hoja zao za kupinga Werandumi kupewa usimamizi wa muda wa mirathi.

Walieleza hawakuwahi kushirikishwa katika uteuzi wa Werandumi ambaye pia tayari amechukua hati za nyumba, kadi za magari, vyeti vya watoto vya kuzaliwa na mali nyingine kadhaa.

Shauri la msingi la kesi hiyo litatajwa Mei 16. Hata hivyo, katika Mahakama ya Wilaya ya Hai, pia kuna maombi ya Zainabu na mtoto wake, kutaka kusimamishwa kwa hatua zote za kuhamisha mali za marehemu ama kuuzwa hadi kesi ya msingi itakapotolewa uamuzi.

Katika Mahakama ya Hai, kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mfawidhi, Devota Msofe ambaye pia tayari Februari 19, alitoa notisi ya kuzuia kuuzwa ama kuhamishwa kwa mali za marehemu hadi kesi ya msingi itakapotolewa uamuzi na imepangwa kutajwa tena Machi 19, mwaka huu.

Bilionea Olomi, ambaye alikuwa anamiliki migodi ya Tanzanite, nyumba, magari na mashamba, alifariki akiwa anatibiwa katika Hospitali ya Aga Khan Jijini Nairobi, Kenya.

Lakini kumeibuka mvutano baina ya ndugu na mke huyo.

Soma zaidi: Kesi ya kugombea mwili wa mchimbaji madini maarufu kunguruma mwezi ujao



Chanzo: mwananchi.co.tz