Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama Kuu yakataa maombi ya watumishi TPA

E80d443454b2f66150fb8f49be92c0f9 Mahakama Kuu yakataa maombi ya watumishi TPA

Thu, 12 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi imetupa maombi ya waliokuwa wafanyakazi 16 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwamba Baraza la Usuluhishi (CMA) lisikilize na kutoa uamuzi kuhusu malalamiko yao.

Charles Daudi na wenzake 15 walipeleka malalamiko CMA baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa TPA kusitisha mikataba yao ya ajira.

Katika shauri hilo lililosikilizwa Mei 2, 2019 na msuluhishi aliyetajwa kwa jina la L, Kokusiima, CMA ilikubaliana na pingamizi la TPA jambo lililosababisha wadai (wafanyakazi hao) kuomba waongezewe muda kwa ajili ya kufungua maombi ya kufanya mapitio ya uamuzi huo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Februari 24, mwaka huu.

Mahakama ilikubali maombi yao na kuwapa siku 14 za kuwasilisha maombi yao ya mapitio. Katika hati ya kiapo iliyoapwa na Daudi kuunga mkono maombi yao, walidai msuluhishi hakuwa na mamlaka ya kukataa kusikiliza malalamiko yao na walikuwa na haki zote za kusikilizwa na baraza hilo.

Akiwasilisha hoja za upande wa walalamikaji Wakili Stela Simkoko alidai wateja wake walisitishiwa ajira zao mwaka 2018 na kwamba CMA ilikuwa na mamlaka ya kuwasikiliza chini ya kifungu 3(a)(ii) cha sheria ya utumishi wa umma sura ya 2098 ya mwaka 2019 na kwamba kwa mujibu wa sheria TPA ni shirika linalomilikiwa na serikali lakini wafanyakazi wake si watumishi wa umma.

Aliendelea kudai kuwa shirika la umma ni tofauti na taasisi ya umma kwa mujibu wa sheria ya mashirika ya umma ambayo inaziondoa taasisi za umma kwenye mashirika hayo.

Alisema tofauti hiyo inawapa uhalali walalamikaji kupeleka malalamiko yao CMA.

Simkoko alisema kigezo kinachotumika kuweka pingamizi kinasimama katika kifungu cha 38A cha sheria ya bandari kilichoongezwa baada ya kufanyiwa marekebisho na kuipa mamlaka kufanya huduma za kiutawala kwa wafanyakazi kwa kufuata sheria ya utumishi wa umma.

Alisisitiza kuwa kabla ya marekebisho walalamikaji hawakuwa chini ya sheria ya utumishi wa umma hivyo wana uhalali wa kupeleka malalamiko yao CMA na kusikilizwa.

Akijibu hoja hizo Wakili wa Serikali, Rehema Mtulia alidai CMA na mahakama hawana mamlaka na kuongeza kuwa sheria ya Mamlaka ya Bandari no 17 ya 2004 kifungu cha 4(1) (a) kinaelezea Mamlaka ya Bandari ni shirika la umma na walalamikaji walisitishiwa ajira mwaka 2018 kwa hati iliyoidhinishwa na serikali kwa hiyo walitakiwa kupeleka malalamiko kwa mujibu wa sheria ya utumishi kabla ya kwenda CMA.

Baada ya kupitia hoja za pande hizo, Jaji alisema TPA wanahusika na vitu muhimu vinavyogusa masuala ya usalama wa nchi hivyo wafanyakazi hawawezi kuchukuliwa kuwa si watumishi wa umma.

Alisema hashawishiki na hoja za walalamikaji kwamba wateja wake si watumishi wa umma hivyo wanatakiwa kupeleka malalamiko yao katika Tume ya Utumishi wa Umma na si kuyapeleka CMA kama walivyofanya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live