Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama Kuu Tanzania yapigilia msumari kifungo cha maisha aliyemlawiti mtoto

71170 Pic+mlawiti

Tue, 13 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imepigilia msumari katika hukumu ya kifungo cha maisha jela inayomkabili mfungwa Riziki Jumanne, baada ya kutupilia mbali rufaa yake ya kupinga adhabu hiyo, badala yake ikaamuru aendelee kutumikia adhabu hiyo.

Hukumu hiyo ambayo Mwananchi limeiona leo Jumanne Agosti 13, 2019, ilitolewa na Jaji Atuganile Ngwala Agosti 9,2019 baada ya kukataa hoja za rufaa za mfungwa huyo pamoja na za Serikali iliyomuunga mkono.

Riziki alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumlawiti mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miaka tisa, mwaka 2016, baada ya kuwa anamrubuni kwa kumnunulia kachori.

Alikata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kupinga hukumu hiyo, hatia na adhabu, akipinga ushahidi wa upande wa mashtaka, kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani.

Alikuwa akidai ushahidi wa shahidi wa pili (mama wa mtoto) huyo hautoshelezi kwani  kuwa mtoto anayedaiwa kutendewa hivyo alipelekwa kwa daktari siku moja baada ya siku ya tukio  iliyodaiwa.

Pia alikuwa akidai upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha umri wa mwathirika kama ni miaka tisa au la wala kuwasilisha vipimo vya vinasaba (DNA).

Pia Soma

Siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, Wakili wa Serikali aliyeiwakilisha Serikali, aliunga mkono rufaa ya mrufani huyo pamoja na mambo mengine akidai hata hati ya mashtaka ilikuwa na kasoro za kisheria, na akaiomba mahakama hiyo imwachie huru.

Hata hivyo, Jaji Atuganile Ngwala aliyesikiliza rufaa hiyo, aliikatalia Serikali akidai kuwa hata kama kulikuwa na kasoro hizo lakini hazikuwa na athari kwani zinaweza kutibika katika vifungu vingine vya kisheria.

Hivyo Jaji Ngwala alikubaliana na hukumu ya Mahakama ya Ilala na akaamuru mshtakiwa aendelee kutumikia adhabu hiyo ya kifungo cha maisha.

“Kwa uzito wa ushahidi huu, nimeridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha mashtaka bila kuacha mashaka. Sioni uzito wa rufaa hii, hivyo inatupiliwa mbali. Mrufani ataendelea na kutumikia adhabu hiyo,” alisema Jaji Ngwala.

Chanzo: mwananchi.co.tz