Mwanza. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza leo Jumatano Julai 24, 2019 imefuta mwenendo mzima wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela waliyopewa watu wa tatu wakiwemo waandishi wa habari wawili.
Pamoja na kufuta mwenendo wa kesi na hukumu, Mahakama pia imeagiza shauri hilo lisikilizwe upya mbele ya Hakimu mwingine.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Mohammed Siani baada ya kukubaliana na rufaa iliyokatwa na waandishi wa habari, Christopher Gamaina na Zephania Mandia na mwenzao Manga Misalaba.
Jaji Siani pia ameagiza usikilizaji upya wa kesi hiyo uzingatie sheria, kanuni, taratibu na haki ya pande zote mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya hukumu hiyo, wakili wa washitakiwa hao, Constatine Mutalemwa ameishukuru mahakama kwa kutenda haki na kuahidi kukamilisha taratibu za kisheria kuwezesha shauri hili kuanza kusikilizwa upya ili wateja wake watendewe haki.
Waandishi hao pamoja na mwenzao tayari wamekaa gerezani kwa miezi mitatu hadi kufikia leo tangu walipohukumiwa.
Pia Soma
- 14 wapandishwa kortini, watuhumiwa kwa utakatishaji fedha
- Mahakama yaelezwa Lissu anaendelea na matibabu
- Nyama ya nyati yampeleka jela miaka 20
Miongoni mwa hoja za rufaa namba 70/2019 zilizokubaliwa na Mahakama ni pamoja na Hakimu aliyesikiliza na kuamua shauri kutozingatia sheria wakati wa ushahidi na baadhi ya mashahidi kutotia saini maelezo yao yaliyotumika kama ushahidi mahakamani.