Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Mahabusu wa Lugola’ apandishwa kizimbani, arudishwa mahabusu

77443 Pic+mahabusu

Fri, 27 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mkazi wa Kahe, Wilaya ya Moshi, Hemed Rajabu (50) ambaye Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliagiza atolewe gerezani, jana alipandishwa kizimbani na kurudishwa gerezani.

Mtuhumiwa huyo amefunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 5 ya 2019 ya kusafirisha kilo 137 za dawa za kulevya aina ya mirungi na kosa hilo anadaiwa kulitenda Julai 18,2019 maeneo ya Kahe.

Jana alifikishwa kortini mbele ya Hakimu Mkazi wa Moshi, Naomi Mwerinde huku wakili wa Serikali kutoka Divisheni ya Taifa ya Mashitaka, Veridian Mlenza akisema upelelezi haujakamilika.

Kutokana na kutokamilika huko kwa upelelezi, hakimu aliiahirisha kesi hiyo ambayo haina dhamana kisheria hadi Oktoba 8 kesi itakapotajwa na mshitakiwa ataendelea kubaki rumande.

Septemba 22, Lugola alimwagiza aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah ambaye sasa ni RPC Morogoro kurudi Kilimanjaro kumtoa mtuhumiwa huyo gerezani.

Waziri alisema Julai 18, Polisi Kilimanjaro walimkamata mshitakiwa huyo, wakati alipokwenda kuangalia mkusanyiko wa watu kufuatia bodaboda kutelekeza furushi la bangi.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Maofisa wa Halmashauri walikuwa wanapita hapo kuelekea kwenye makusanyo, lakini Mmbaga akawa wa kwanza kufika eneo hilo akitokea nyumbani polisi wakamkamata,”alisema Lugola.

Lugola alisema polisi walimbambikia kesi ya kukutwa na dawa za kulevya na taarifa zilipomfikia aliagiza atolewe mara moja mahabusu lakini hadi juzi alikuwa bado hajatolewa.

Hata hivyo, mawakili , wameeleza kuwa mtu pekee mwenye mamlaka ya kisheria ya kumfutia mtu kesi iliyopo mahakamani ni Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) tena kwa utashi wake mwenyewe.

Wakili wa kujitegemea, Frank Mushi alisema RPC kama RPC au polisi yoyote hana mamlaka ya kumfutia mtu kesi iliyopo mahakamani bali anaweza kuagiza kufungwa kwa jalada la uchunguzi.

“Polisi wajibu wao unaishia pale wanapokusanya ushahidi na kupeleka jalada kwa DPP. DPP akiona kuna ushahidi anafungua kesi na ni yeye anaweza kuiondoa hatua yoyote,”alieleza.

Kifungu cha 90(1)(C) cha CPA kinaeleza kuwa DPP anaweza kutoendelea na mwenendo wowote wa shauri la jinai na kifungu cha 91(1) kinasema DPP anaweza kufuta mashitaka katika hatua yoyote.

Kwa mujibu wa wakili huyo, hakuna mahali ambapo sheria hiyo imempa mamlaka RPC kumtoa mtu mahabusu isipokuwa ni DPP tu ndiye mwenye mamlaka ya kumtoa Mmbaga gerezani.

Chanzo: mwananchi.co.tz