Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maeneo yanayoongoza kwa utakatishaji fedha

59865 Pic+fedha

Mon, 27 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya juhudi kadhaa za kukabiliana na utakatishaji fedha, Serikali imebainisha sekta zinazoongoza kwa uhalifu huo sambamba na makosa yanayojirudia, ripoti inaonyesha.

Kwa mujibu wa ripoti ya utakatishaji fedha na ugaidi ya mwaka 2016 (National money laundering and terrorism financing risks assessment report 2016) iliyotolewa hivi karibuni na Idara ya Udhibiti Fedha Haramu (FIU) ya Wizara ya Fedha na Mipango, biashara ya magari, nyumba, maduka ya kubadilishia fedha na madini ndiyo maeneo yanayoongoza kwa utakatishaji fedha.

Ripoti hiyo inasema, watu wanaopata fedha chafu kutokana na uhalifu tofauti, huziwekeza kwenye maeneo hayo ili kuzitakatisha. Ukosefu wa vitambulisho hasa vya Taifa kwa wananchi wengi, ripoti inasema ni mwanya unaotumiwa vyema na wahalifu hao.

Licha ya maeneo hayo yanayowavutia watakatishaji fedha nchini, ripoti hiyo imebainisha makosa sita yaliyogundulika, kuchunguzwa na kuhukumiwa. Takwimu zilizokusanywa kutoka vyombo vya ulinzi na usalama zinabainisha makosa, thamani ya mali zilizokamatwa na kutaifishwa hata faini iliyolipwa na wahusika.

Ufisadi na rushwa, ukwepaji kodi, dawa za kulevya, uuzaji na umiliki wa noti bandia, uchimbaji na biashara haramu ya madini pamoja na ujangili na umiliki wa nyara za Serikali, ripoti inasema ndio makosa yanayohusiana na utakatishaji fedha.

“Maeneo hayo bado hayasimamiwi vya kutosha hivyo kutoa nafasi kwa watakatishaji fedha kufanya watakavyo bila kuingiliwa na vyombo vya usalama,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Pia Soma

Biashara ya magari, ripoti inasema ni miongoni mwa sehemu zinazokimbiliwa na watakatishaji kutoka na watu wengi kupenda kumiliki magari ama kwa biashara au matumizi ya familia.

“Magari hasa ya kifahari hununuliwa na watakatishaji kufanikisha shughuli zao za kihalifu. Biashara hii ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi lakini matumizi ya fedha taslimu ni mwanya unaotumiwa na wahalifu hawa,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Usimamizi mdogo uliopo kwenye biashara nyumba na viwanja, ripoti inasema unatoa mwanya kwa watakatishaji kujificha kwenye sekta hiyo. Matukio machache huripotiwa kwenye eneo hilo licha ya miamala mikubwa inayofanyika.

Taasisi za fedha yakiwamo maduka ya kubailishia fedha, benki za biashara, Saccos na Vicoba ni eneo jingine ambalo linaelezwa kutumika kufanikisha uhalifu huo. Bahati nasibu, casino na aina nyingine za bahati nasibu ni maeneo mengine ambako fedha haramu huelekezwa.

Uchimbaji na biashara haramu ya madini, ripoti inasema ni eneo linalopendwa na watakatishaji fedha kutokana na urahisi wa kuuza madini.

“Kwa Tanzania, ni rahisi kwa mtu yeyote kununua madini ya thamani kubwa hata kutoka mamlaka husika bila kushukiwa. Mara nyingi, biashara hii hufanyika kwa fedha taslimu,” inasema ripoti hiyo.

Kukabiliana na uhalifu huo, ripoti inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Utakatishaji Fedha (Anti-Money Laundering Act) ya mwaka 2006 na Sheria ya Utakatishaji Fedha na Mwenendo wa Makosa Yake (Anti-Money Laundering and Proceeds of Crime Act) ya mwaka 2009 ili kuweka vifungu vitakavyoongeza adhabu kwa wahalifu.

Chanzo: mwananchi.co.tz