Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maelezo ya mshtakiwa yakwamisha kesi ya kigogo TRA

42867 KIGOGOPIC Maelezo ya mshtakiwa yakwamisha kesi ya kigogo TRA

Fri, 22 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka umedai bado hawajakamilisha kuandaa maelezo ya mshtakiwa katika kesi inayomkabili Ofisa Msaidizi wa Forodha, kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA), Godfrey Mapuga.

Mapuga anayekabiliwa na shtaka moja la kumiliki mali zenye thamani ya Sh721 milioni, ambazo haziendani na kipato chake cha sasa na cha zamani.

Wakili Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Vitalius Peter amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Salum Ally, kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa Maelezo ya Awali (PH).

Peter amedai bado hawajakamilisha kuandaa maelezo ya mshtakiwa hivyo waliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ili waweze kukamilisha.

"Tunaahidi tarehe hiyo tutakuwa tumekamilisha na siku hiyo tutaendelea na shahidi wa kwanza," amedai Peter.

Wakili wa utetezi, Mluge Fabian amedai ni mara ya pili wanaahirisha shauri hilo hivyo aliuomba upande wa mashtaka kukamilisha kuandaa maelezo ya mshtakiwa.

"Mteja wangu anakuja hapa akitokea mkoa wa Kagera na yupo kikazi kwani kuandaa maelezo ya mshtakiwa ni kazi ya siku moja tu haichukui wiki nane," amedai Fabian.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Ally amesema ucheleweshwaji huo unaolalamikiwa na upande wa utetezi ni kweli na hiyo ni mara ya pili upande wa utetezi wanakuja na hoja hiyo.

"Upande wa mashtaka mjitahidi kukamilisha kuandaa maelezo ya mshtakiwa ili tuepushe ucheleweshwaji wa kesi hii," amesema Ally.

Hakimu Ally ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 16, 2019 itakapokuja kwa ajili ya maelezo ya awali. Hata hivyo, mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Mapunga anadaiwa kumiliki viwanja vitatu pamoja nyumba ya moja ya ghorofa, ambavyo haviendani na kipato chake, katika kesi ya jinai namba 13/2019.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Aprili Mosi, 2011 na Julai 19, 2016 eneo la  Ubungo.

Mapuga akiwa kama mtumishi wa umma, anadaiwa kumiliki nyuma moja ya ghorofa, iliyopo Goba Manispaa ya Ubungo, yenye thamani ya Sh698.9 milioni ambayo haiendani na kipato chake cha sasa na cha zamani.

Pia katika kipindi hicho, mshtakiwa anadaiwa kumiliki kiwanja kimoja ambacho hakijasajiliwa kilichopo  Mbezi Juu, Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam chenye thamani ya Sh7 milioni.

Vile vile, anadaiwa kumiliki ardhi ambayo haijasajiliwa iliyopo eneo la Kigamboni, yenye thamani ya Sh6 milioni.

Mapuga anadaiwa kumiliki kiwanja ambacho hakijasajiliwa kilichopo Goba, chenye thamani Sh9.5 milioni na kufanya idadi ya mali anazodaiwa kumilikiambazo haziendani na kipato chake cha sasa na cha zamani kufikia Sh721.4 milioni

Mali za mamilioni zampeleka kortini ofisa TRA



Chanzo: mwananchi.co.tz