Arusha. Idara ya Ukaguzi na Udhibiti wa Utoroshwaji Madini katika mpaka wa Namanga mkoani Arusha nchini Tanzania imekamata madini yenye thamani ya Sh1.3 bilioni mwaka kuanzia mwaka 2018 hadi sasa.
Ofisa mfawidhi wa idara hiyo, Arnold Kishashu ametoa taarifa hiyo leo Jumatano Julai 3, 2019 katika kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa taasisi 14 za Serikali zinazo fanya kazi katika kituo cha pamoja cha forodha.
Amesema madini hayo yenye uzito wa kilo 63.645 yamekamatwa mwaka 2018/2019.
Akizungumza baada ya taarifa hiyo, mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe ameeleza kuridhishwa na utendaji wa idara hiyo na kuagiza Mamlaka ya Mapato Namanga kuwapa ofisi katika jengo lao.