Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaraja ya juu yalivyogeuka maficho ya wahalifu Dar

Manze Daraja maarufu la Manzese jijini DSM

Mon, 28 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya barabara jijini Dar es Salaam zimejengewa madaraja ya juu, ili kuwawezesha watu wanaovuka barabara kupita kwa usalama, kuepuka ajali.

Kivuko cha muda mrefu ni kile cha Manzese katika barabara ya Morogoro, maarufu kama Manzese Darajani kilichojengwa mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Hata baada ya barabara za Morogoro na Kawawa kuboreshwa kwa kuwekewa njia za magari yaendayo haraka, yameongezwa madaraja mengine ya wapita kwa miguu, likiwemo la Ubungo, Kimara mwisho na Mbezi karibu na kituo cha basi cha Magufuli na Kinondoni Morocco.

Daraja lingine lipo Buguruni na jingine lipo barabara ya Bagamoyo eneo la Tangibovu.

Lengo la ujenzi wa madaraja hayo ni kuongeza usalama kwa wananchi wanaotembea kwa miguu, lakini sasa baadhi ya wananchi wanayatumika kinyume cha malengo hayo.

Uhalifu

Advertisement Madaraja hayo licha ya kuwa msaada kwa wanaotembea kwa miguu, yamekuwa kivutio huku baadhi wakiyatumia kupigia picha, kufanya biashara na sasa wengine wameyageuza kuwa vituo vya uhalifu.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walieleza kupatwa na masahibu kwenye madaraja hayo, akiwemo Said Juma aliyeporwa simu juzi, saa 2:00 usiku kwenye daraja la Morocco baada ya kuvamiwa na vijana wawili huku mmoja kati yao akiwa ameshika panga.

“Walinisimamisha na mmoja akanikwapua simu na wakaanza kukimbia. Sikuwa na nguvu ya kuwafuata kwani walikuwa wawili, mmoja alikuwa na panga,” alisema Juma.

Naye Alphonse Kisiga, mkazi wa Mbezi alielezea namna alivyoporwa begi lake kwenye daraja la Mbezi wakati anawahi kwenda stendi ya mabasi Magufuli kupanda basi la kwenda mkoani Iringa.

“Nilikutana na vijana watatu waliokuwa wanajifanya madalali wanaokatisha tiketi, baada ya kuchukua begi langu walianza kukimbia kuelekea standi na baadaye sikuwaona tena,” alisema na kuongeza kuwa hali hiyo inachangiwa na daraja kutokuwa na taa.

Kutokana na uhalifu, baadhi ya watembea kwa miguu hawapendi kupitia kwenye madaraja hayo, badala yake wanavuka moja kwa moja barabarani, hali inayohatarisha usalama wao.

Ukweli huo unadhihirishwa na Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani kanda ya Dar es Salaam (ZTO), Abdi Issango aliyesema maeneo ya madaraja kumekuwa na ajali nyingi za waenda kwa miguu zinazosababishwa na watu kutoyatumia madaraja wakihofia kuporwa vitu na vibaka.

Aliyataja madaraja hayo kuwa ni pamoja na daraja la Mbezi Mwisho, Manzese na Buguruni.

“Abiria wengi wanagongwa kwenye daraja la Mbezi Mwisho, pale pabaya sana, lile daraja limewekwa ili watu wavuke wakitoka stendi waende wakapande daladala kituoni, lakini wengi wanaona wakipandisha daraja watapoteza muda, pale wanagongwa na wengine wanapoteza maisha,” alisema Issango.

Kwa upande wa maeneo ya kwenye vivuko, Issango alisema ajali hazitokei mara nyingi kutokana na madereva wengi kujua sheria za usalama barabarani, kuzizingatia na pia kuonekana kwa alama za vivuko na ushirikishwaji wa jamii.

Aliyataja maeneo hatarishi kwa ajali za pikipiki ni maeneo yote ya makutano ya barabara, ikiwemo kwenye mataa ya barabarani.

“Barabara ya Morogoro inaongoza kwa pikipiki wengi kugongwa hasa maeneo ya Magomeni Mapipa, Mbezi mwisho pale kwenye mataa, stendi ya Magufuli, Mbezi kwa Yusuph na katika barabara ya Mandela pamoja na Buguruni. Barabara ya Nyerere pale Kamata, Jet, Gongo la Mboto, Barabara ya Kilwa pale mataa ya Uhasibu,” alisema.

Issango aliyataja maeneo mengine kuwa ni Kwa Azizi Ally, Mbagala Rangitatu na barabara ya Bagamoyo alilitaja eneo la mataa ya Morocco, mataa ya Mwenge, Bunju na Temeke ni eneo la Serengeti. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni alipoulizwa kuhusu uhalifu kwenye madaraja hayo, alisema hajawahi kupokea malalamiko ya aina hiyo.

“Sijawahi kusikia mtu anaporwa Morocco ambako ni jirani na kituo cha Polisi Oysterbay na kuja kituoni kutoa taarifa. Ni vizuri wakaja ili tuone namna nzuri ya kuwasaidia,” alisema Kingai.

Pia alitoa maelekezo kwa watu wanaofanya vitendo hivyo kuacha mara moja, kwani wakiingia kwenye mkono wa Polisi wasilaumu mtu yeyote.

Tanroads

Akizungumzia kutokamilika kwa madaraja hayo, hasa kutokuwa na taa nyakati za usiku, Meneja wa Tanroads Dar es Salaam, Mhandisi Haruni Senkuku alisema wanafuatilia vivuko vyote vinavyolalamikiwa, ikiwemo Buguruni na Morocco ili kuweka taa hizo.

“Kwa madaraja yote yaliyopo kwenye barabara nane bado ujenzi wake unaendelea, hivyo tunaomba wawe na subira na baada ya kukamilika lazima kutakuwa na taa za kuimarisha usalama kwa watumiaji,” alisema Senkuku.

Kuhusu vivuko vya pundamilia, alisema maeneo hatarishi wanayogongwa watu mara kwa mara wakipata taarifa wanachukua hatua kwa uharaka kujua changamoto inayosababisha.

Alitaja miongoni mwa sababu zinazosababisha changamoto hiyo ni barabara kupanuliwa au alama kufutika.

Kwa upande wa vivuko, alisema wanachofanya ni kuvihuisha mara kwa mara, ili matarajio yaliyowekwa kwenye barabara hizo yaende kama yalivyopangwa, huku akitoa wito kwa watumiaji kama wanaona changamoto waziweke wazi.

“Lakini upande wa pili ni usimamizi wa sheria, kwa hiyo lazima tusaidiane na sekta mbalimbali katika kulinda usalama wa watumiaji na miundombinu yenyewe,” alisema Senkuku.

Alisema madaraja ya Mbezi na Kimara bado ujenzi unaendelea, lakini kwenye vivuko vya kawaida kuna alama za zebra.

Starehe

Wakati wengine wakilalamikia vitendo vya uporaji, uchunguzi wa Mwananchi umebaini pia kuwepo kwa shughuli za starehe katika madaraja hayo, hususan katika madaraja ya Manzese na Buguruni, hasa nyakati za sikukuu.

Wapo wanaopiga picha kwa kumbukumbu ya baadaye na kutokana na maendeleo ya teknolojia, wapo wanaotumia simu zao kufanya hivyo, huku wengine wakihitaji huduma za wapigapicha.

Mwananchi limeshuhudia katika daraja la Manzese nyakati za jioni watu wakiwa wamefurika na wapigapicha wakijipatia biashara kwa watu wanaotaka kupata matukio ya kumbukumbu.

Mmoja wa wapigapicha aliyejitambulisha kwa jina moja la Ngosha alisema kipindi cha sikukuu na siku za mwisho wa wiki huwa ni kipindi cha neema, kwani hupata watu wengi wanaohitaji kupigwa picha.

“Kwa siku za kawaida naweza kuingiza Sh10,000 hadi 15,000 lakini kipindi cha sikukuu naweza kupata Sh20,000 hadi 30,000 inategemea na wahitaji. Picha moja nauza Sh1,000,” alisema.

Katika daraja la Buguruni napo kumegeuka kuwa sehemu ya biashara ndogo kama maputo, vinywaji, ice cream, mayai na wengine wakifanya shughuli ya upigaji picha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live