Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabosi mamlaka ya maji kortini kesi ya bil 5/-

54f2e7eb4615ccc32233941557622155 Mabosi mamlaka ya maji kortini kesi ya bil 5/-

Mon, 6 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imewafikisha mahakamani watu saba wakiwemo viongozi sita wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Jiji Arusha (AUWSA), wanaotuhumiwa kujipatia isivyo halali shilingi bilioni 5.3

Miongoni mwa washitakiwa katika kesi hiyo ya matumizi mabaya ya madaraka, kula njama na kujipatia fedha hizo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Ruth Koya.

Washitakiwa wengine ambao ni wafanyakazi wa mamlaka hiyo ni Benedict Kitigwa, James Mwambona, Steven Msenga, Godfrey Macha na Juma Mkwawa. Mshitakiwa mwingine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiure Engineering Ltd, Omari Kiure mkazi wa jijini Arusha.

Akisoma mashitaka hayo Mbele ya Hakimu, Herieth Mtenga wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, mwishoni mwa wiki,Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Violet Machali alidai kuwa washitakiwa kwa pamoja walitenda makosa manne ya uhujumu uchumi na kujipatia shilingi 5,310,823,214.

Machali alidai kuwa, shitaka la kwanza linawahusu washitakiwa wote na akadai kuwa, walitenda kosa hilo kati ya Desemba, 2017 na Oktoba mwaka 2018 katika eneo la Jiji la Arusha.

Alidai kuwa washitakiwa walikula njama kupitia mradi wa maji wa kanda na kuipatia manufaa kampuni ya ujenzi ya Kiure Engineering Ltd ya jijini humo bila kuzingatia taratibu za ununuzi. Machali alidai kuwa shitaka la pili ni matumizi mabaya ya madaraka na linamhusu mshitakiwa wa kwanza, Ruth Koya.

Alidai kuwa wakati akiwa mtumishi wa umma na akifahamu ni kosa kisheria aliiwezesha kampuni ya Kiure Engineering LTD kupata mkataba wa ujenzi wa ofisi za kanda za AUWSA hivyo kampuni hiyo ikapata manufaa ya shilingi bilioni 5.3 kinyume cha kifungu cha 36(5) cha sheria ya ununuzi ya mwaka 2011.

Machali alidai kuwa shitaka la tatu na la nne linawahusu mshtakiwa wa 1,2,3,4 na 5 ambao ni Ruth Koya, Benedict Kitigwa ,James Mwambona ,Steven Msenga na Godfrey Macha.

Alidai kuwa kati ya Desemba 2017 na Oktoba 2018 kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao na kuiwezesha kampuni ya Kiure Engineering Ltd ipate manufaa ya shilingi bilion 5.3.

"Mh hakimu sisi upande wa Jamhuri hatuna pingamizi la dhamana tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya washitakiwa kuwasomea maelezo ya awali kwani upelelezi wa shauri hili umekamilika"alisema Machali

Hakimu Mtega alisema dhamana kwa washtakiwa ipo wazi na kwamba watapaswa kuwa wadhamini wawili akiwemo mtumishi wa umma mwenye kitambulisho na barua ya utambuzi kutoka kwa mwajiri wake. Alisema mdhamini angepaswa kusaini bondi ya mali isiyohamishika yenye thamani ya shilingi milioni 20.

Washitakiwa hao kwa pamoja wanatetewa na wakili, Robert Rogati na wote walitimiza masharti ya dhamana hivyo wapo nje hadi watakaposomewa maelezo ya awali Septemba 9 mwaka huu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz