Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabishano ya kisheria yaibuka kortini kesi ya Dk Pima

HUKUMU Mabishano ya kisheria yaibuka kortini kesi ya Dk Pima

Fri, 14 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabishano makali ya kisheria yameibuka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake wawili baada ya mawakili wa Serikali kuweka pingamizi, wakitaka Mahakama isipokee nyaraka zinazodaiwa kutoka kampuni ya Cherry General Supply and Services ya jijini Arusha.

Mabishano hayo yameibuka leo Alhamisi Julai 13, 2023 katika shauri hilo linalosikilizwa na hakimu mkazi, Serafini Nsana baada ya kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 14, 2023 kwa ajili ya kutoa uamuzi mdogo wa pingamizi hilo.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022 mbali na Dk Pima,watuhumiwa wengine ni aliyekuwa Mwekahazina wa Jiji hilo,Mariam Mshana na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango,Takwimu na Ufuatiliaji,Innocent Maduhu.

Mabishano hayo yalidumu kwa zaidi ya saa tatu na yalianza baada ya Maduhu akiongozwa na wakili wake, Sabato Ngogo kuiomba Mahakama ipokee nyaraka hizo “delivery note” kama kielelezo Mahakamani hapo.

Akiongezea hoja hiyo ya Wakili Ngogo, ameieleza Mahakama kuwa Aprili 17, 2023 waliwasilisha notisi kwa upande wa Jamhuri kuomba nyaraka halisi.

Amesema notisi hiyo waliiwasilisha kuomba nyaraka halisi chini ya vifungu vya 67(1) na 68 vya sheria ya ushahidi, sura ya 6 marejeo ya mwaka 2022.

Maombi ya kupokelewa nyaraka hizo yalipingwa na mawakili wa Serikali waandamizi, Hebel Kihaka na Timotheo Mmari walioomba kutopokea nyaraka hizo kwani hazijakidhi matakwa ya sheria hiyo.

Akiwasilisha hoja za pingamizi, Wakili Kihaka aliieleza Mahakama kuwa wanapinga kupokelewa nyaraka hizo na kuwa licha ya kupewa notisi hiyo lakini hawajahi kuwa nazo wala vyombo chunguzi (polisi na Takukuru) hawajawahi kuwa nazo na kuomba Mahakama isipokeee nyaraka hizo kama kielelezo.

“Tumeeleza wazi Mahakamani, hii Jamhuri haijawahi kuchukua nyaraka hizo lakini hata ushahidi uliotolewa na Jamhuri unaonyesha wazi namna nyaraka mbalimbali zilivyokuwa zikichukuliwa kwa utaratibu upi na mashahidi walieleza nyaraka zote zilichukuliwa kwa hati ya kuchukulia nyaraka na nakala mojawapo kubaki kwa mchukuliwa,” amesema.

“Tunaamini nyaraka hizi ni za kutengenezwa tu au kwa maana nyepesi zimeghushiwa na ndiyo sababu kuu hata mmiliki wa hiyo Cherry au maofisa wake hawakuonyeshwa nyaraka hizi kuwadhirishia kama ni kweli waliwasilisha ule mzigo unaodaiwa kuwa walitoa. Tunaamini kabisa ni kuwasingizia hao Cherry na kuwanyima haki yao ya kusikilizwa kuhusiana na tuhuma hizo kama wao ni waandaaji wa hizi nyaraka,” alisema.

Wakili Mmari aliiomba mahakama kutopokea nyaraka hizo kwani hazijakidhi vigezo vya kisheria.

Awali, Maduhu aliieleza Mahakama kuwa alilipa fedha taslimu Sh103 milioni kwa kampuni hiyo ambayo baada ya malipo, walipeleka malighafi katika kiwanda cha matofali Njiro, kinachomilikiwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya kutengeneza matofali.

Alidai kuwa waliopokea malighafi hizo kiwandani humo ni Moses Joseph na Brenda Mbagga. Aliongeza kuwa walitoa hizo “delivery notes” na kuomba Mahakama izipokee kama kielelezo.

Baada ya mabishano hayo, Hakimu Nsana aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 14,2023 kwa ajili ya uamuzi mdogo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live