Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maafisa 'feki' Ikulu wakutwa na kesi ya kujibu

Hukumu Pc Data Maafisa 'feki' Ikulu wakutwa na kesi ya kujibu

Wed, 22 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemkuta na kesi ya kujibu mshtakiwa Joshua Kamalamo (37) na mwenzake, Yahaya Kapalatu (31) wanaodaiwa kujitambulisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), kuwa wao ni maofisa kutoka Ofisi ya Raisi- Ikulu, Idara ya Usalama wa Taifa, wakati wakijua uongo.

Hiyo ni baada ya Serikali kufunga ushahidi wao wa mashahidi wanne na vielelezo viwili, vilivyowasilishwa mahakamani hapo.

Kamalamo na Kapalatu wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 99/2021 yenye mashtaka mawili ya kujitambulisha kwa DPP na kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka (DDPP) kuwa wao ni maofisa kutoka Ofisi ya Raisi, Idara ya Usalama wa Taifa, jambo ambalo ni uongo.

Uamuzi huo umetolewa leo, Februari 22, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi iwapo washtakiwa wanakesi ya kujibu au laa.

Akisoma uamuzi huo, hakimu Kabate amesema amepitia ushahidi wa mashahidi hao wa upande wa mashtaka na kuona kuwa washtakiwa wote wanayo kesi ya kujibu, hivyo anatakiwa kujitetea.

Hata hivyo, washtakiwa hao wameieleza Mahakama hiyo kuwa watajitetea wenyewe kwa njia ya kiapo na hawatakuwa na mashahidi.

Hakimu Kabate baada ya kusikiliza maelezo ya washtakiwa hao, ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 28, 2023 itakapoitwa kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea.

Hata hivyo, washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana.

Awali, Wakili wa Serikali, Adolf Verandumi alidai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya uamuzi na upande wa mashtaka wapo tayari.

Katika kesi ya msingi, Kamalamo peke yake, inadaiwa Juni 11, 2021 katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka nchini ( NPS) ilizopo katika jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani, jiji hapa, alijitambulisha kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DDPP), Joseph Pande kuwa anatoka Ofisi ya Rais, Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Siku hiyo Kamalamo alimwambia Pande kuwa amepewa maelekezo kutoka kwa Rais kuwa wasiendelee na majadiliano ya kuimaliza kesi (Ple Bargaining) katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2017 inayomkabili Harbinder Seth na wenzake, mpaka hapo watakapopewa maelekezo mengine.

Shtaka la pili, linawakabili washtakiwa wote ambapo wanadaiwa Juni 12, 2021, katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka nchini ( NPS) ilizopo katika jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani, jiji hapa, Kamalamo na Kapalatu walijitambulisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Slyvester Mwakitalu kuwa wanatoka Ofisi ya Rais, Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Siku hiyo Kamalamo na Kapalatu, wanadaiwa walimueleza DPP kuwa wamepewa maelekezo kutoka kwa Rais kuwa wasiendelee na majadiliano ya kuimaliza kesi (Ple Bargaining) katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2017 inayokuwa inamkabili Harbinder Seth na wenzake, mpaka hapo watakapopewa maelekezo mengine, Jambo ambalo wanajua kuwa ni uongo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live