Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MO: Nilipotekwa wananchi wengi waliniombea

2d34a17ab7ccfc7a8528a5f3e2832b15 MO: Nilipotekwa wananchi wengi waliniombea

Mon, 26 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MFANYABIASHARA Mohamed Dewji (MO), amekumbuka siku tisa alizotekwa huku akieleza wananchi kuwa ana deni kubwa kwao kwa kuwa katika kipindi hicho watu mbalimbali bila kujali hali zao, kiuchumi walikuwa wakimuombea.

Aidha, amemuahidi Rais Samia Suluhu Hassan kuwa katika kipindi chake cha uongozi kwa miaka minne anatarajia kuongeza ajira kwa vijana kutoka 31,000 hadi 100,000.

Dewji alisema hayo jana Dare s Salaam wakati akizungumza na wanafunzi wanufaika wa ufadhili wa masomo unaotolewa na mfuko wa Mo Dewji Foundation unaotumika kusaidia wanafunzi mbalimbali wenye mahitaji ya kutimiza ndoto zao kusoma katika vyuo vikuu.

Akizungumza na wanufaika hao, Dewji alisema mwanzo alikuwa akitoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba kuingia sekondari, lakini akaona aongeze wigo kwa wanaokwenda vyuo mbalimbali vya elimu.

Alisema anafanya hayo yote si kwa sababu nyinginezo, bali amekuwa na deni kubwa kwa Watanzania hasa anapokumbuka kuanzia mwaka 2018 alipotekwa kwa siku tisa akiwa amefungwa macho, mikono na miguu akisimamiwa na bunduki na kujua kuwa angekufa.

“Lakini dua na sala za Watanzania wote bila kujali itikadi zao za dini waliniombea na Mungu alisikiliza sala za Watanzania na hatimaye nikarejea, sasa ni hai,” alisema Dewji na kuhoji kuwa ni lini watu maskini walimuombea tajiri.

Alisema Watanzania wote walimuombea, na hilo ndilo deni kubwa alilonalo na kwa kuwa anaipenda nchi yake, anajua kuwa ipo siku atakufa hapahapa na atazikwa nchini Tanzania kwa kuwa hana pengine pa kwenda.

Hata hivyo alisema ana imani kubwa na Rais Samia kwa kuwa tangu ameingia madarakani ameonesha njia na kwa wafanyabiashara kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo ya nchi.

Kuhusu wanufaika, alisema alianzisha mfuko huo mwaka 2016 ambapo hadi sasa umewanufaisha zaidi ya wanafunzi 100,000 kwa kusoma fani mbalimbali katika vyuo vikuu nchini ili kuboresha maisha ya Watanzania masikini na kufikia ngazi za kuwa na maendeleo. Alisema alishatumia zaidi ya Sh bilioni moja kwa kipindi cha miaka mitano kwa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi na kuwasisitiza kuwa wapatapo ajira, wajitahidi kufanya kazi kwa bidii na watambue kuwa hahitaji chochote kutoka kwao.

Aliwataka wanufaika hao kuendelea kumuombea kwa bidii kwa kuwa yuko katika wakati mgumu hata katika klabu yake ya michezo ya Simba.

Awali, mwanafunzi wa Shahada ya Mafuta na Gesi, Miriam Ibrahim, alipongeza jitihada zinazofanywa na Dewji katika kufadhili wanafunzi wenye uhitaji kwa kuwa wanafikia ndoto zao wakitambua kuwa elimu ni nguzo ya maendeleo.

Alisema ufadhili huo umefungua ndoto zao na kwa sasa vyuo vinavyonufaika vimefikia zaidi ya 10 kutoka vyuo viwili ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Chanzo: www.habarileo.co.tz