Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: hahidi aeleza alivyogundua mwili mtoni

54759 Pic+scolastica

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Jackson Kileo, ambaye ni shahidi wa 18 katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa shule ya Scolastca, Humphrey Makundi (16), ameeleza namna alivyougundua mwili wa mtoto huyo Mto Ghona mwaka 2017.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kuuawa usiku wa Novemba 6, 2017 na baadaye mwili wake kutupwa Mto Ghona uliopo umbali wa mita takribani 300 kutoka shule ya Scolastica.

Washitakiwa katika kesi hiyo inayovuta hisia za watu wengi ni mlinzi wa shule hiyo Hamis Chacha, mmiliki wa shule Edward Shayo na mwalimu wa zamu Laban Nabiswa ambao wamekana shitaka hilo.

Akiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Omary Kibwana kutoa ushahidi wake jana, shahidi huyo wa 18 alidai kuuona mwili huo Novemba 10, 2017 wakati akivuka mto kuelekea mji wa Himo.

Mbele ya Jaji Firmin Matogolo wa Mahakama Kuu anayesikiliza kesi hiyo mjini Moshi, shahidi huyo alidai aliposogelea eneo hilo aliona mwili wa mtu ukielea mtoni.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, ulikuwa wa jinsia ya kiume na ulikuwa umevaa nguo ya bukta, fulana ya ndani (vesti) na soksi na kwamba ulikuwa umelalia tumbo.

Related Content

Shahidi huyo alieleza kuwa baada ya kuona hivyo, aliwatumia ujumbe mfupi wa simu (SMS), balozi aliyemtaja kwa jina la Kyara na mwenyekiti aliyemtaja kwa jina la Robert Lekule.

Alieleza kuwa baada ya hapo polisi walifika eneo la tukio na walishirikiana na baadhi ya wananchi ambao aliwataja kuwa ni Paul Minja na mmoja kwa jina la Mmasai kuupoa mwili huo kutoka majini.

Kulingana na ushahidi huo, mwili wa marehemu ulikuwa umeshaanza kuvimba na polisi waliutoa na kuuweka kwenye machela na wananchi waliofika hapo walipata fursa ya kuangalia mwili huo.

Baadaye ulichukuliwa na polisi ambao walisema wanaupeleka hospitali ya Mawenzi na kueleza kuwa hawezi kusema kwa uhakika Korongo lililopo upande wa Himo katika mto lina ukubwa gani.

Katika hatua hiyo, Wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande alisimama na kuiomba mahakama ikubali ushahidi wa shahidi huyo uahirishwe ili wamuite shahidi wa 19 ambaye ushahidi wake unashabihiana.

Wakili huyo alisema kwa kuwa ushahidi wa shahidi wa 18 na wa 19 unafanana, ni vyema shahidi wa 19 akatoa ushahidi wake ili watakapokwenda eneo la tukio, wasiisumbue Mahakama kurudi mara mbili.

Hata hivyo jopo la mawakili wa utetezi, Elikunda Kipo`ko anayesaidiana na David Shillatu, Wakisa Sambo na Patrick Paul, walipinga wakitaka hilo lifanyike baada ya pande zote kufunga ushahidi.

Jaji Matogolo aliiahirisha kesi hiyo saa 6:45 mchana hadi saa 7:30 mchana ili aweze kupitia hoja za mawakili wa pande zote mbili na hatimaye kutoa uamuzi mdogo juu ya mabishano hayo ya kisheria. Jaji Matogolo alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka ambapo shahidi wa 19, Inspekta Waziri Tenga alipanda kizimbani kutoa ushahidi wake.



Chanzo: mwananchi.co.tz