Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA :Tafrani yaibuka hukumu mauaji ya mwanafunzi wa Scolastica

61293 Scolapic

Tue, 4 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Staili ya kuaga ya mmiliki wa shule ya Scolastica, Edward Shayo, jana ilizua tafrani kwenye viwanja vya Mahakama Kuu Moshi na kusababisha polisi kutumia nguvu kumdhibiti baba mzazi wa mtoto aliyeuawa.

Jackson Makundi ambaye ni baba wa Humphrey Makundi aliyeuawa usiku wa Novemba 6,2017 na maiti yake kutupwa mto Ghona, alifika mahakamani hapo saa 9:40 alasiri na kukosa nafasi ya kuingia ndani ya mahakama.

Ndani na nje ya chumba cha mahakama kulikuwa na idadi kubwa ya watu kiasi kwamba, baadhi ya wasikilizaji walilazimika kusimama ndani na nje ya mahakama.

Baada ya Mahakama kumalizika na washitakiwa wakiwa wanapelekwa katika gari la polisi ili kupelekwa Gereza la Karanga, ndipo Shayo alipowapungia mamia ya watu huku akiwaaga.

Ni katika kipindi hicho alimuona baba wa marehemu na kutamka maneno kuwa, “Makundi damu ya mtoto wako hainihusu”, maneno yaliyoibua hasira kwa mzazi na kutaka kwenda kumshambulia.

“Unasemaje?” alisikika Makundi akiuliza huku akielekea kwenye gari ya polisi hali iliyoibua kelele za kurushiana maneno kati ya ndugu, jamaa na marafiki wa makundi na wale wa upande wa Shayo.

Pia Soma

“Yeuwi ana bastola huyo,” walisikika baadhi ya watu wakisema huku wakipiga mayowe wakimaanisha baba wa marehemu ana bastola ingawa hata hivyo hakuwa nayo.

Kulitokea tafrani kubwa ndipo polisi waliingilia kati na kutumia nguvu kumuingiza Makundi katika gari yake.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, mama wa marehemu, Joyce Makundi aliishukuru mahakama kwa kutenda haki lakini akaomba Waziri wa Elimu kuifutilia shule ya Scolastica kwa undani.

“Namshukuru Mungu, ameonekana tangu mwanangu alivyouawa na namrudishia Mungu sifa na utukufu wake kwa sababu hata dunia imejua ukweli na haki imetendeka.

“Nimshukuru kipekee Jaji kwa jinsi alivyoongozwa na Mungu na sheria hadi kutoa hukumu hii, lakini nawashukuru watu wote waliotuunga mkono tangu mwanzo wa tukio hili hadi leo tunapohitimisha,” alisema mama huyo.

Aliwashukuru pia polisi waliofanya uchunguzi wa tukio hilo pamoja na mawakili wa Serikali walioendesha kesi hiyo, akisema walitumia weledi na weledi wao umeisaidia Mahakama kutenda haki.

Mawakili wa Serikali walioendesha kesi hiyo ni Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande Mawakili wa Serikali waandamizi, Abdalaha Chavulla na Omary Kibwana na Wakili wa Serikali, Lucy Kyusa.

Hata hivyo, alimuomba Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako kuifuatilia shule ya Scolastica akisema tangu tukio litokee, haijachunguzwa mwenendo wake wala kuchukulia hatua za kinidhamu.

Ushahidi aina tatu ulivyowatia hatiani

Ni ushahidi wa aina tatu tu ndio ulimshawishi Jaji Firmin Matogolo kumhukumu adhabu ya kifo, mshitakiwa Hamis Chacha kwa kumuua mwanafunzi wa shule ya Scolastica, Humphrey Makundi.

Ushahidi huohuo ndiyo uliowaingiza mmiliki wa shule, Edward Shayo na mwalimu wa nidhamu. Laban Nabiswa ambao wamehukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa kuficha taarifa za mauaji.

Ushahidi huo ni maelezo ya ungamo ya mshitakiwa namba moja,Chacha aliyoyatoa kwa mlinzi wa amani, mawasiliano ya simu ya washitakiwa na ungamo la mdomo la Chacha kuhusu panga alilotumia.

Akisoma adhabu baada ya kuchambua ushahidi na kuzingatia maombolezo ya washitakiwa, Jaji Matogolo alisema kosa la mauaji ya kukusudia kwa mujibu wa sheria ni moja nayo ni adhabu ya kifo.

“Kwa mshitakiwa wa kwanza (Chacha), adhabu iliyowekwa kwa mujibu wa sheria ni moja tu nayo ni kifo. Kwa hiyo utanyongwa hadi ufe. Nimefungwa mikono siwezi toa adhabu mbadala,”alisema Jaji.

Kuhusu mshitakiwa Shayo maarufu kama Kingsize na Nabiswa, Jaji Matogolo alisema wao walipaswa kushiriki kulea watoto lakini wakashiriki kuficha taarifa za mauaji ya mwanafunzi wao, Humphrey.

“Nimesikiliza maombolezo yaliyotolewa na mawakili wenu pamoja na nyinyi wenyewe lakini adhabu ndogo hutolewa kulingana na kosa na adhabu hiyo ilenge kumrekebisha mhalifu,”alisema Jaji.

Jaji Matogolo alieleza katika hukumu yake hiyo kuwa adhabu hiyo pamoja na kumrekebisha mhalifu, lakini lazima ifinye ili kutoa funzo kwa mhalifu na jamii ili isifikirie kutenda kosa kama hilo.

Washitakiwa walivyomwaga chozi kortini

Kwa mujibu wa Jaji Matogolo, kosa lililoko mbele ya mahakama ni mauaji ya kukusudia ya mtoto na mwanafunzi wa Scolastica hivyo Shayo na Nabiswa watatumikia kifungo cha miaka minne gerezani.

Kabla ya kuwapa adhabu hiyo, Jaji alitoa fursa kwa kila mshitakiwa kusema chochote ambapo mshitakiwa Chacha aliomba mahakama imuonee huruma kwa kuwa ana familia inayomtegemea.

Hata hivyo Shayo kwa upande wake, alianza kububujikwa na machozi akisema hajawahi kutenda kosa na kwamba damu ya mtoto huyo haiko katika mikono yake wala mikono ya watoto wake.

Mshitakiwa huyo kama alivyo Nabiswa, aliiomba mahakama imuonee huruma na kumwachia kwani katika maisha yake hajawahi kutenda kosa lolote na ni mara ya kwanza anasimama mahakamani.

Awali akichambua ushahidi uliowatia hatiani washitakiwa, Jaji Matogolo alisema hakuna ubishi kuwa mwanafunzi huyo alikufa kifo kisicho cha kawaida na maiti yake kukutwa mto Ghona.

“Swali hapa ni jinsi mwili ulifikaje mto Ghona? Hili jibu tutalipata kwenye maelezo ya ungamo ya mshitakiwa wa kwanza (Chacha) ambaye alieleza bayana namna alivyomfukuza marehemu,”alisema.

Jaji Matogolo alirejea maelezo hayo ambayo Chacha alieleza namna alivyomfukuza marehemu, kumpiga kwa bapa la Panga hadi alipoanguka na kupasuka paji la uso na kuendelea kumshambulia.

Baada ya kuona mtu huyo ameshakufa, Chacha ndipo akawaita washitakiwa wenzake kwa simu nao walifika eneo la tukio na ndipo pendekezo la kutupa mwili huo mtoni lilipotolewa na Shayo.

Jaji Matogolo alisema japokuwa Chacha alijitetea kuwa alitoa maelezo hayo baada ya kuteswa sana, utetezi huo ni wa uongo kwani maelezo hayo aliyatoa kwa hiyari na kueleza kila kitu kilivyotokea.

Kuhusu kielelezo namba 7 ambacho ni mawasiliano ya simu, Jaji Matogolo alisema washitakiwa hawakatai kuwasiliana usiku wa tukio, lakini wanaeleza mawasiliano yao hayakuhusu tukio hilo.

“Mawasiliano yao (ya simu) waliyafanya kutimiza lengo lao ovu. Swali hapa la kujiuliza sasa ni nani alimuua Humphrey Makundi? Mshitakiwa katika ungamo lake anasema yeye ndio alimpiga”

“Mshitakiwa huyo amewataja mshitakiwa wa pili (Shayo) na mshitakiwa wa tatu (Nabiswa) kwamba aliwaita eneo la tukio usiku huo lakini si kwa kumshambulia (marehemu),”alisema Jaji na kuongeza;-

“Je, wakati anawapigia simu, marehemu alikuwa ameshafariki au alikuwa hai na alikufa baada ya kutupwa mtoni?. Nimepitia ushahidi nimeona hakufa kwa kutupwa mtoni bali kwa kupigwa kichwani”

Jaji Matogolo alisema hakuna ushahidi wowote uliotolewa mahakamani unaoonyesha dhamira ya pamoja ya washitakiwa ya kutenda mauaji ila wanaunganishwa na ungamo kutupa mwili mtoni.

“Hakuna ushahidi ulioletwa ukionyesha mshitakiwa wa pili (Shayo) na wa tatu (Laban) walishiriki kuua isipokuwa walijitokeza tu baada ya mauaji hivyo walishiriki jinai ya kuficha taarifa za mauaji.

Kuhusu ushahidi wa Panga, Jaji Matogolo alisema kitendo cha Chacha kuwapeleka polisi hadi eneo alilokuwa ameficha panga, ni kukiri kosa kwa mdomo ambako kulitosha kumtia hatiani.

Katika hukumu yake hiyo, Jaji Matogolo ameamuru pia simu zote sita za washitakiwa zitaifishwe na Serikali kwa vile zilitumika katika kosa kwa kuwasiliana washitakiwa na kuitana eneo la tukio.

Hukumu hiyo ilisomwa kuanzia saa 3:36 asubuhi hadi saa 9:50 alasiri, lakini iliahirishwa kwa nusu saa saa 7:45 mchana hadi saa 8:15 mchana ili kuwapa muda mawakili wa utetezi kuandaa maombolezo.

Chanzo: mwananchi.co.tz