Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Simu ya mshtakiwa yapokewa mahakamani

52689 Pic+scolastica

Wed, 17 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mahakama Kuu imepokea simu aliyokuwa akiitumia Hamis Chacha kama kielelezo katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Scolastica, Humphrey Makundi.

Simu hiyo iliwasilishwa mahakamani na shahidi wa 16 wa upande wa mashtaka Koplo Enock kutoka ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai (RCO) mkoani Kilimanjaro jana mbele ya Jaji Firmin Matogolo wa Mahakama Kuu.

Shahidi huyo alidai kuwa Novemba 17, 2017 aliitwa ofisi ya RCO ili aende shule ya Scolastica kuwakamata watu wawili wanaodaiwa kuhusika katika mauaji, ambao ni mshtakiwa wa kwanza, Chacha na Mchamungu Kiwelu ambaye ni mlinzi mwenzake. Wote ni walinzi wa shule hiyo.

Alidai baada ya kumkamata Chacha alichukua simu yake aina ya Tecno iliyokuwa kwenye mfuko wake wa suruali. Mshtakiwa huyo alikiri kuwa ni mali yake na kisha kwenda naye kituo cha kikuu cha polisi.

Alidai simu hiyo ilikuwa na laini moja ya Vodacom pamoja na namba mbili za utambulisho (imei).

Baada ya kutoa ushahidi wake, aliomba simu ipokewe kama kilelelezo cha upande wa mashtaka na hakukuwa na pingamizi.

Related Content

Katika kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia namba 48 ya 2018 inadaiwa kuwa Novemba 6, 2017, Humphrey aliuawa kisha mwili wake kuokotwa Mto Ghona, takriban mita 300 kutoka eneo la shule hiyo.

Alidai baada ya kumkamata mshtakiwa huyo siku iliyofuata walimrejesha tena walikomkamatia ambako aliwaonyesha panga lililokuwa katika chumba cha walinzi wa shule hiyo.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa na wakili mkuu wa Serikali, Joseph Pande akisaidiwa na mawakili waandamizi Abdallah Chavula, Omari Kibwana na Lucy Kyusa huku ule wa utetezi ukiwa na mawakili Elikunda Kipoko, Wakisa Sambo, Patrick Paul na David Shilatu.

Sehemu ya mahojiano ya shahidi huyo na wakili wa upande wa mashtaka, Lucy Kyusa ilikuwa ifuatavyo:

Wakili Kyusa: Tarehe 18/11/2017 ulipokea taarifa gani?

Shahidi: Mchana nikiwa ofisini nilipata taarifa kutoka kwa Inspekta Fredy tumpeleke Chacha Himo akatuonyeshe kielelezo alichokitaja.

Wakili Kyusa: Nini kilifuata?

Shahidi: Nilimfuata Central Inspekta Fredy akanambia tunatakiwa twende Himo mhalifu akatuonyeshe panga.

Wakili Kyusa: Nini kiliendelea?

Shahidi: Tulimtoa lockup (mahabusu), tukaelekea naye Himo Shule ya Scolastica.

Wakili Kyusa: Nini kiliendelea?

Shahidi: Hamis Chacha alichukuwa panga lililokuwa kwenye kibanda cha walinzi na kumkabidhi Inspekta Fredy.

Baada ya upande wa mashtaka kumaliza mahojiano na shahidi huyo, mawakili wa utetezi nao walimhoji shahidi huyo.

Wakili Shilatu: Ieleze mahakama ni kweli tarehe 18/11/2017 ulienda Scolastica kukamata kielelezo?

Shahidi: Nilienda kuonyeshwa kielelezo.

Wakili Shilatu: Unafahamu PGO?

Shahidi: Ndio

Wakili Shilatu: Unajua panga lilitakiwa kuchukuliwa alama za vidole?

Shahidi: Mimi sifahamu

Wakili Shilatu: Nitakua sahihi kusema kielelezo hiki hakina mahusiano ya moja kwa moja na Chacha?

Shahidi: Sio sahihi

Wakili Shilatu: Unafahamu ni wajibu wenu (polisi) kulinda kielelezo?

Shahidi: Inategemea

Wakili Shilatu: Ni kweli panga ulilosema ni la Chacha hamkulilinda?

Shahidi: Sio kweli

Wakili Shilatu: Wewe ulishiriki kumhoji Chacha?

Shahidi: Sikushiriki

Wakili Shilatu: Ulijuaje Chacha ameua?

Shahidi: Ni taarifa ambazo tulipewa

Wakili Shilatu: Wewe ulimuona Chacha akiua?

Shahidi: Sikumuona

Kesi hiyo itaendelea leo



Chanzo: mwananchi.co.tz