Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Saa 100 za kesi mauaji mwanafunzi

53202 Pic+scolastica

Sat, 20 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Takribani saa 100 za usikilizaji mfululizo wa kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Sekondari ya Scolastica, Humphrey Makundi, zimeshuhudia mashahidi 17 wa mashtaka wakitoa ushahidi na kukabidhi vielelezo 11.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kuuawa usiku wa Novemba 6, 2017 na baadaye mwili wake kutupwa Mto Ghona, uliopo umbali wa takribani mita 300 kutoka katika shule hiyo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia ni Hamis Chacha, mlinzi wa shule hiyo, mmiliki wa shule, Edward Shayo na aliyekuwa mwalimu wa zamu siku ya tukio hilo Laban Nabiswa, ambao wamekana shtaka hilo.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Firmin Matogolo katika Mahakama Kuu mjini hapa ilianza Aprili 2 kusikilizwa kwa siku 11 na kuahirishwa Aprili 16 hadi Aprili 29.

Kwa siku hizo, kesi hiyo ilikuwa ikianza kati ya saa 3:30 na saa 4:00 asubuhi, na kuahirishwa kati ya saa 11 jioni na saa 2:30 usiku. Hesabu zinaonyesha kwa siku hizo ilisikilizwa si chini ya jumla ya saa 100.

Vielelezo vilivyopokewa na mahakama ni pamoja na panga linalodaiwa kutumika katika mauaji hayo, ripoti ya uchunguzi wa kifo na ya vinasaba (DNA).

Related Content

Ripoti ya DNA ilitolewa na shahidi wa 12, mkemia wa Serikali, Hadija Mwema, ikieleza sampuli zilizochukuliwa kwenye mwili wa Humphery zilioana na zile za baba yake, Jackson Makundi na mama, Joyce.

Vielelezo vingine ni ripoti ya mawasiliano ya simu zinazodaiwa za washtakiwa pamoja na maelezo ya ungamo ya mshtakiwa Chacha anayodaiwa kuyatoa kwa mlinzi wa amani Novemba 20, 2017.

Pia simu za washtakiwa zilipokewa kama vielelezo. Kabla ya kupokewa kwa maelezo hayo, mahakama iliingia katika hatua ya kesi ndani ya kesi ili kujiridhisha kama uchukuaji wake ulifuata sheria na iwapo mshtakiwa aliyatoa kwa hiari.

Jopo la mawakili wa utetezi pamoja na mshtakiwa mwenyewe waliyapinga maelezo hayo kwa sababu kuu mbili.

Mosi, walidai uchukuaji wake haukuzingatia matakwa ya sheria na hoja ya pili iliegemea kuwa mshtakiwa huyo alifanyiwa mateso na ukatili mkubwa na polisi ili kuandika maelezo hayo.

Akitoa ushahidi wake katika kesi ndani ya kesi, mshtakiwa huyo alidai kufanyiwa mateso mbalimbali ikiwamo kuchomwa pasi sehemu ya uume na kuingiziwa chupa ya bia kwenye sehemu ya haja kubwa.

Pia alidai kabla ya kuandika maelezo, polisi aliowataja kwa majina walimwingizia sindano ndefu kwenye uume wake, kumpiga kwa fimbo na kumlaza uchi katika chumba kilichokuwa na maji.

Hata hivyo, jopo la mawakili wa mashtaka likiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande anayesaidiana na mawakili wengine watatu lilipinga vikali madai hayo.

Katika kesi ndani ya kesi, shahidi wao wa kwanza ambaye ndiye aliyeandika maelezo hayo, Irene Mushi, alieleza kuwa mshtakiwa alikuwa na afya njema wakati akitoa maelezo hayo mbele yake.

Jaji Matogolo alitupilia mbali pingamizi la mawakili wa utetezi na kukubaliana na hoja za mawakili wa Serikali kuwa hakuna ukiukwaji wa sheria na mshtakiwa aliyatoa maelezo hayo kwa hiari.

Katika uamuzi wake mdogo, jaji alieleza kuwa hoja kuwa mshtakiwa aliteswa na polisi aliowataja haikuwekwa mbele ya polisi hao walipotoa ushahidi wao wala kuuliza kuhusu kumtesa.

Pia akasema kwa mazingira ya kawaida na kwa mateso aliyoyapata asingeshindwa kunyoosha mkono na kumweleza hakimu alipofikishwa kortini kwa mara ya kwanza.

“Kuna maswali ya kujiuliza. Kama kweli aliteswa hivyo hasa lile jeraha la moto aliloionyesha mahakama ilipokwenda faragha, alipokelewaje magereza?” alihoji Jaji Matogolo katika uamuzi wake.

“Kuna ushahidi wake mshtakiwa alikamatwa pamoja na mlinzi mwenzake, swali la kujiuliza, kwanini yeye tu ateswe? Uongo wa mshtakiwa unaweza kuunga mkono ushahidi wa mashtaka.”

Hata hivyo, jaji alisema kupokewa kwa nyaraka (kielelezo kama yalivyo maelezo hayo ya ungamo) ni kitu kimoja na haina maana kikipokewa ndicho pekee kitazingatiwa katika hukumu.

Akisoma neno kwa neno la maelezo hayo, Irene amemnukuu mshtakiwa akieleza kuwa Novemba 6, 2017 saa 2:58 usiku, alisikia kishindo cha mtu akishuka (ukuta) na aliamua kufuatilia.

Sehemu ya maelezo hayo ya ungamo yaliyopokewa mahakamani kama kielelezo yanaeleza kuwa mshtakiwa huyo anadaiwa kueleza kuwa alimulika tochi kuelekea eneo hilo na mtu huyo alianza kukimbia na yeye kumkimbiza na kwa vile alikuwa na silaha aina ya panga, alimpiga nalo kwa ubapa.

“Nilimpiga bapa mgongoni na aliendelea kukimbia na nikakimbizana naye na kuna sehemu alifika na kuanguka chini na alipasuka kwenye paji la uso. Baada ya hapo akawa katulia,” ananukuliwa mshtakiwa katika maelezo hayo.

“Nikampiga bapa la pili na ndio mauti yalipomkuta palepale. Nilimpigia simu mwalimu Laban nikamwambia kuna mtu nimemkimbiza lakini sijui kama ni mwanafunzi au mtu wa nje.

“Ndipo mwalimu Laban ambaye ni mwalimu wa nidhamu akaja. Palepale akaniuliza nimeshampigia mkuu wa shule nikamjibu kuwa nilishampigia mzee wa shule, mzee Shayo anakuja.

“Baada ya hapo nilimwambia mwalimu Laban inawezekana huyu mtu kazirai tumbebe tumpeleke hospitali, mwalimu Laban akadai tumsubiri mzee Shayo afike. Mzee Shayo alivyofika ndio nikamueleza.

“Mzee Shayo akamuuliza mwalimu Laban unamfahamu huyu mtu, Laban alijibu naona kavaa sare za shule lakini siwezi kumfahamu kwa muda huu.

“Mzee Shayo akasema kama humfahamu kwa muda huu ukatupwe huko mtoni labda ni kibaka na mimi na mwalim Laban tulienda kumtupa huko mtoni.”

Kesi hiyo iliahirishwa Jumatano ya Aprili 17 hadi Aprili 29 itakapoendelea kusikilizwa kwa upande wa mashtaka kuita mashahidi zaidi.



Chanzo: mwananchi.co.tz