Moshi. Hamis Chacha, mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi Humphrey Makundi, jana alipata wakati mgumu hadi kushindwa kufahamu jina la baba mkwe wake.
Mshtakiwa huyo alijikuta katika wakati mgumu zaidi alipoonyeshwa maelezo aliyoyaandika Novemba 14,2017 shuleni wakati polisi walipofika kuchunguza kupotea kwa mwanafunzi huyo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Chacha ambaye ni mlinzi wa shule, Edward Shayo mmiliki wa shule akiwa mshtakiwa wa pili na Laban Nabiswa ambaye ni mshtakiwa wa tatu.
Hayo yalijitokeza wakati Wakili wa Serikali mwandamizi, Abdalah Chavulla akimhoji mshtakiwa huyo kutokana na ushahidi wake wa utetezi alioutoa kwa kuongozwa na wakili wake, David Shillatu.
Katika ushahidi wake wa msingi, mshtakiwa huyo alieleza kuwa Novemba 6,2017 ambayo ni siku ambayo mwanafunzi huyo aliuawa, akiwa doria saa 2 usiku alimkurupusha mtu akakimbilia uraiani.
Alidai mara baada ya mtu huyo kukurupuka, alimulika tochi kuona kama kuna watu wengine, lakini hapakuwepo na mtu mwingine eneo hilo na kusisitiza kuwa yeye hakumkimbiza mtu huyo.
Habari zinazohusiana na hii
- MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA : Hivi ndivyo ilani ya mmiliki wa Scolastica inavyoeleza kortini
- MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Awashushia lawama polisi akidai kuteswa kwa siku tatu
- MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA : Washtakiwa wana kesi
Hata hivyo, wakati akihojiwa jana na Wakili Chavulla aeleze ni maelezo yapi ni sahihi kati ya aliyosema baada ya kumkurupusha hakumkimbiza au alimkimbiza hadi nyumba ya wageni ya BBC.
Sehemu ya mahojiano kati ya shahidi huyo na Wakili Chavulla yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Chavulla: Nilikusikia hapa ukisema una mke?
Shahidi: Ni kweli mheshimiwa
Wakili Chavulla: Anaitwa nani?
Shahidi: Anaitwa Dorina
Wakili Chavulla: Dorina nani?
Shahidi: Jina la baba yake silifahamu. Ni jina la Kijaluo. Majina ya Kijaluo ni magumu
Wakili Chavulla: Ulimuoa mkeo ukiwa na miaka mingapi?
Shahidi: Sikumbuki ila nilimuoa 2014
Wakili Chavulla: Ulimuoa kimila au ndoa ya Kikristo kanisani?
Shahidi: Ndoa ya kimila
Wakili Chavulla: Unapotaka kuoa ni lazima uwaambie wazazi wako nataka kuoa binti wa fulani, si ndio?
Shahidi: Ndio
Wakili Chavulla: Uliwatajia (wazazi wake) majina ya wazazi wa Dorina?
Shahidi: Mie niliwaambia nataka kuoa
Wakili Chavulla: Jina la baba mkwe wako unalisahau kwa sababu ni gumu, ndivyo unavyotaka mahakama iamini hivyo?
Shahidi: Kweli silikumbuki ni jina gumu
Wakili Chavulla: Namba ya mke wako ni ngapi?
Shahidi: Yeye simu yake ilichukuliwa na mtoto wake akawa anatumia simu ya mdogo wake?
Wakili Chavulla: Ni namba ngapi hiyo simu ya mdogo wake?
Shahidi: Siikumbuki ila inaanza na 0716 na kuishia na 22
Baada ya kueleza hivyo, Wakili Chavulla aliomba apatiwe kielelezo namba 7 cha mahakama ambayo ni taarifa ya mawasiliano ya simu ya washtakiwa waliyoyafanya usiku wa Novemba 6,2017.
Katika kielelezo hicho, shahidi huyo aliitaja namba ya mkewe na kueleza kuwa siku ya tukio alimpigia simu saa 2:57 usiku na kusisitiza kutokana na upendo huwa wanawasiliana mara kwa mara.
Wakili Chavulla: Unamfahamu mshtakiwa wa tatu (Laban)?
Shahidi: Ndio ni Mwalimu Laban
Wakili Chavulla: Mwalimu Laban anamfahamu mkeo?
Shahidi: Hapana hamfahamu
Wakili Chavulla: Mwalimu Laban ana mawasiliano na mkeo?
Wakili Chavulla: Mimi nakuambia mwenye hiyo namba unayodai ni mkeo anamjua Laban?
Shahidi: Sio kweli
Wakili Chavulla akampa tena kielelezo namba 7 na kumtaka aeleze namba hiyo kama iliwasiliana na Laban na baada ya kusoma ilionyesha Laban aliwasiliana na mwenye namba hiyo zaidi ya mara nne.
Wakili Chavulla: Hebu iangalie hii nyaraka (akampa) utuambie kuanzia tarehe 7.11.2017 hadi 13.11.2017 ni wakati gani uliwasiliana na huyo mke wako?
Shahidi: Sikuweza kuwasiliana naye tena.
Wakili Chavulla: Sasa nakuambia mwalimu Laban alikuwa anawasiliana na mkeo, lakini wewe mwenye mke hujawasiliana naye kwa siku zote hizo, ndio unataka mahakama iamini hivyo?
Shahidi: Mimi siwezi kujua kama wanawasiliana
Wakili Chavulla: Nakuambia wewe ni mwongo. Nikikuambia mwenye hiyo namba sio mke wako bali mwenye namba hiyo anaitwa Justine Eliezer na yuko Himo na biashara zake zinajulikana.
Shahidi: Siwezi kujua alitumia kitambulisho gani kusajili.
Mwanafunzi Humphrey Makundi (16), aliyekuwa akisoma kidato cha pili anadaiwa kuuawa usiku wa Novemba 6,2017 na mwili wake kutupwa katika Mto Ghona uliopo mita 300 kutoka shuleni hapo.
Kesi hiyo itaendelea leo