Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Mshtakiwa apinga ushahidi wa mshtakiwa mwenzake kortini

56397 PIC+SCOLASTICA

Thu, 9 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Laban Nabiswa, mshtakiwa wa tatu katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa shule ya Scolastica, Humphrey Makundi, amepinga ushahidi uliotolewa na mshtakiwa mwenzake, Hamis Chacha.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Edward Shayo ambaye ni mmiliki wa shule hiyo, mlinzi wa shule, Chacha na Nabiswa ambaye ni mwalimu wa nidhamu ambao wamekana shitaka hilo.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kuuawa usiku wa Novemba 6, 2017 na baadaye mwili wake kutupwa katika Mto Ghona uliopo mita 300 kutoka katika shule hiyo na baadaye ukazikwa na Manispaa ya Moshi.

Katika utetezi wake, mshtakiwa wa kwanza, Chacha aliiambia mahakama kuwa simu ya kwanza kuipiga usiku wa saa 2:57 wa Novemba 6, 2017 ilikuwa ni ya mkewe aliyemtaja kwa jina la Norina.

Akiongozwa na wakili wake, David Shillatu kutoa utetezi wake, Chacha alieleza kuwa amekuwa akitumia namba hiyo kumpigia simu mkewe ambaye yupo Tarime mkoani Mara.

Alieleza kuwa alipokamatwa Novemba 17, 2017 na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi, alikutana na mlinzi mwenzake, Mchamungu Kiwelu ambaye walikamatwa pamoja kwenye chumba chenye maji.

Habari zinazohusiana na hii

Hata hivyo, akitoa utetezi wake wakati akihojiwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Abdalah Chavulla, mshtakiwa huyo, Nabiswa alisema ushahidi wa Chacha kuhusu namba ya mkewe si sahihi.

Sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Chavulla na mshtakiwa huyo yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Chavulla: Bwana Chacha wakati tunamhoji alisema ana mke anampenda sana anaitwa Dorina na Chacha akazitaja namba zake. Hebu iambie mahakama, wewe Dorina unamfahamu?

Mshtakiwa: Mheshimiwa Jaji huyo Dorina simfahamu.

Wakili Chavulla: Mheshimiwa Jaji tunaomba kielelezo P7. (Baada ya kupewa), shahidi hebu tusaidie. Kwa mujibu wa Chacha alituambia aliongea na namba hiyo (akaitaja) usiku wa tarehe 6.11.2017 mara mbili na wakati huu ndio alimkurupusha mtu. Wewe unasemaje ni kweli ni mke wa Chacha?

Mshtakiwa: Mheshimiwa Jaji nina mashaka na hilo.

Wakili Chavulla: Shahidi tuambie mwenye hiyo namba ni nani?

Mshtakiwa: Baada ya hilo swali kuibuliwa hapa nilitumia hiyo call log (mawasiliano ya simu) nili-analyse (kufanya uchambuzi) nahisi ni namba ya mwalimu lakini kwa sababu ni muda mrefu siwezi kukumbuka.

Wakili Chavulla: Kwa hiyo analysis yako, utakubaliana na mimi kuwa Chacha ni mwongo hii siyo namba ya mkewe?

Mshtakiwa: Ndio maana nina mashaka kwa sababu hiyo namba ilikuwa miongoni mwa namba za walimu niliowatumia message (ujumbe) kwa sababu mimi ni katibu.

Wakili Chavulla: Nitakuwa sahihi nikisema ilikuwa inatumika Himo siyo nje ya Himo?

Mshtakiwa: Ni mpaka printout yake ije tujue

Wakili Chavulla: Kwani mke wa Chacha ni mwalimu pale Scolastica?

Mshtakiwa: Angekuwa mwalimu pale ningelikuwa namfahamu. Simfahamu mke wa Chacha.

Wakili Chavulla: Ni sahihi nikikuambia namba ya Chacha aliyokuwa anawasiliana nayo hukuishia tu kuitumia meseji bali ulikuwa unaipigia na mnaongea?

Mshtakiwa: Ni kweli mheshimiwa nilikuwa nawasiliana naye.

Wakili Chavulla: Na kwa hicho kitendo cha kutumiana meseji ni lazima atakuwa mwalimu wa Scolastica?

Mshtakiwa: Ndio mheshimiwa Jaji ni sahihi, lakini siyo lazima awe mwalimu maana kuna subordinate staff (kada ya chini) mpaka niangalie

Wakili Chavulla: Bila kujali ni mwalimu lakini atakuwa mwana Jumuiya ya Scolastica?

Mshitakiwa: Sahihi mheshimiwa Jaji.

Wakili Chavulla: Chacha katika ushahidi wake mara mbili hapa alisema mtu pekee aliyekutana naye kule polisi siku ile ya tarehe 17.11.2017 ni Mchamungu, wewe leo unasema ulionana naye kwenye chumba ulipopelekwa kutoa maelezo yako. Isaidie mahakama nani anasema ukweli?

Mshtakiwa: Hicho nilichokisema ndicho sahihi.

Awali akihojiwa na Wakili Elikunda Kipoko anayemtetea mshtakiwa wa pili, Shayo, mshtakiwa huyo alidai usiku wa Novemba 17, 2017 saa 4, polisi walimpeleka kwenye chumba cha mateso.

“Maaskari walinipiga sana. (huku akianza kububujikwa na machozi). Walinipiga sana hadi nikajikojolea. Nikawaambia sijui chochote muulizeni Mchamungu kama nilitoka shuleni,” alieleza.

Kwa mujibu wa mshtakiwa huyo, polisi hao walikuwa wakimpiga na kumueleza kuwa Chacha amewaeleza kwamba baada ya kuua, alimpigia simu yeye na wakasaidiana kuutupa mwili mtoni.

Mshtakiwa huyo alidai polisi walitaka aunge mkono maelezo ya Chacha na aliwaambia hawezi kukiri jambo ambalo hajafanya na Inspekta Waziri Tenga akasema lazima amshtaki kwa mauaji.

Itaendelea kesho



Chanzo: mwananchi.co.tz