Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Mmiliki Scolastica abubujikwa machozi kortini

56181 Shahidi+pic

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mshtakiwa wa pili, Edward Shayo (65) katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Scolastica, Humphrey Makundi jana alibubujikwa machozi karibu muda wote wakati akitoa ushahidi.

Akihojiwa na upande wa mashtaka, mshtakiwa huyo aliomba ufanyike uchunguzi juu ya muamala wa Sh500,000 anazodaiwa kumtumia ofisa wa Polisi siku moja baada ya tukio la mauaji.

Kwa mujibu wa kielelezo P7, Novemba 7, 2017 saa 4:37 mshtakiwa huyo anadaiwa kutuma kiasi hicho kwenda kwa namba ya Inspekta Juma Idd wa kituo cha Himo.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande ulidai fedha hizo zilitumwa ili kuficha taarifa za mauaji ya mwanafunzi huyo anayedaiwa kuuawa Novemba 6, 2017 na mwili wake kutupwa Mto Ghona, mita 300 kutoka katika shule hiyo na uligunduliwa Novemba 10, 2017.

Akiongozwa na Wakili Gwakisa Sambo kutoa ushahidi, Shayo alidai kuwa Novemba 6, 2017 saa 11 jioni alikuwa ofisini kwake.

Huku akibubujikwa na machozi hadi Jaji Firmin Matogolo anayesikiliza kesi hiyo kuingilia kati na kumsihi aache kulia, aliiambia Mahakama kuwa ilipofika saa moja usiku aliondoka na kuelekea Njiapanda ambako alikutana na rafiki yake aitwaye Kimambo katika Baa ya Giraffe.

Habari zinazohusiana na hii

Alidai kuwa ilipofika saa tatu usiku aliondoka hapo na kuelekea hoteli yake ya African Flower, Himo na akiwa njiani, Chacha alimpigia simu kumjulisha kuwa kuna mtu amemkurupusha.

“Kwenye saa 3:09 usiku Hamis Chacha alinipigia simu akaniambia nimemkurupusha mtu shuleni. Nilimpigia director (mkurugenzi) nikamweleza na kumuambia afuatilie hiyo taarifa,” alieleza.

Shahidi huyo alieleza kuwa alifika African Flower saa 3:20 usiku na kuwakuta marafiki zake pamoja na fundi wa TV wakinywa kahawa huku wakitazama taarifa ya habari ya BBC ya Kiswahili.

Kati ya saa 4:20 na saa 4:30 usiku, aliagana nao na kuelekea nyumbani, lakini akapita shuleni Scolastica na kuegesha gari lake kwani shule hiyo iko jirani na nyumbani kwake.

Alieleza kuwa saa 4:41 usiku alimpigia Chacha simu na kumtaka atumie mfereji wa umwagiliaji unaopita shuleni hapo, kumwagilia ukoka uliokuwa umepandwa katika uwanja wa shule hiyo.

Alisema taarifa za kupotea kwa mtoto huyo alizipata Novemba 12, 2017 na Novemba 15, 2017 alikamatwa na polisi na kupelekwa Kituo cha Polisi Himo na baadaye kituo kikuu Moshi.

“Pale Himo polisi nilikutana na Jackson Makundi ambaye ni baba wa mtoto akaniambia kama hutanionyesha mtoto wangu nitakuonyesha. Hapohapo niliwekwa chini ya ulinzi. Nilimuuliza yule askari wa counter (mapokezi) kwa nini nawekwa chini ya ulinzi, nimefanya kosa gani akasema hakuna kosa ila wananiweka chini ya ulinzi kwa sababu za usalama wangu.”

Alieleza kuwa alipohamishiwa Moshi, alinyimwa dhamana na baadaye hali yake ya kiafya ilidhoofu kutokana na matatizo ya kisukari, moyo na shinikizo aliyonao.

Polisi walimpeleka Hospitali ya KCMC alikolazwa hadi Novemba 27, 2017 alipopelekwa mahakamani na kufunguliwa shtaka la mauaji.

Kufika hapo, hali ya kulia iliongezeka na Jaji Matogolo alimtaka ajikaze na ushahidi wake ni muhimu kwani haki inatafutwa.

“Sikumfahamu huyo mtoto sura wala jina lake kipindi chote cha uhai wake. Wala sikusikia kuna tatizo limetokea tarehe 6.11.2017 hata Jackson nilimwambia damu ya mwanaye haiko mikononi mwangu.

Shahidi huyo aliulizwa pia anazungumziaje maelezo ya ungamo wa Chacha ambaye alikuwa ni mfanyakazi wake kukiri kosa la mauaji na kueleza kuwa walishirikiana naye na Laban, akasema yeye hakushiriki.



Chanzo: mwananchi.co.tz