Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA : Mawakili walivyowasilisha majumuisho

57108 Pic+scolastica

Mon, 13 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Scolastica, Humphrey Makundi umewasilisha majumuisho ya kesi hiyo na kueleza kuwa umeweza kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa wote.

Hata hivyo kwa upande wao, mawakili wa utetezi katika majumuisho yao wameeleza kuwa upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa na kuiomba mahakama iwaachie huru.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni mlinzi wa shule hiyo, Hamis Chacha, mmiliki wa shule, Edward Shayo maarufu kwa jina la “Kingsize” na mwalimu wa nidhamu, Laban Nabiswa ambaye ni raia wa Kenya.

Hayo yamo katika majumuisho yaliyowasilishwa mahakamani kwa njia ya maandishi Ijumaa iliyopita na mawakili baada ya Jaji Firmin Matogolo anayesikiliza kesi hiyo kutaka itumike njia hiyo.

Jopo la mawakili wa Jamhuri ambao waliita mashahidi 18 na vielelezo 12 liliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande akisaidiwa na Abdalah Chavulla, Omary Kibwana na Lucy Kyusa.

Katika majumuisho hayo, mawakili hao wa upande wa mashtaka walitaja hoja nne zilizotakiwa kujibiwa ambazo ni pamoja na kama mwanafunzi huyo alitoweka shuleni Scolastica Novemba 6,2017.

Habari zinazohusiana na hii

Hoja nyingine ni kama mwili ulioopolewa Mto Ghona ulikuwa wa mwanafunzi huyo, kama mwanafunzi huyo alikufa kifo kisicho cha kawaida na kama washtakiwa ndio walimuua mwanafunzi huyo.

Kujibu hoja ya kwanza, mawakili hao wameeleza kuwa mwanafunzi Raymond Mollel aliyekuwa akilala kitanda kimoja na marehemu, alimueleza Laban siku hiyo Humphrey hakulala katika kitanda hicho.

Pia wameeleza kuwa katika uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi Novemba 14,2017, mshtakiwa Chacha aliwaeleza polisi kuwa usiku wa Novemba 06, 2017 alimkurupusha mtu kwenye uzio.

Mbali na ushahidi huo, lakini mshtakiwa Laban katika ushahidi wake alieleza kuwa Novemba 7, 2017 ndio alithibitisha Humphrey hakuwepo shuleni kwa kuwa siku hiyo hakufanya jaribio la Fizikia.

Kuhusu hoja kama mwili uliopolewa Mto Ghona ni wa Humphrey, mawakili hao wamesema upo ushahidi wa mashahidi wanne wa Jamhuri walioeleza kuwa Novemba 10, 2017 mwili wa mtu uliopolewa mtoni. Lakini pia upo ushahidi wa mashahidi sita kwamba Novemba 17,2017, mwili huo ulifukuliwa katika makaburi ya Karanga ambapo mashahidi hao waliutambua ndio ule ule ulioopolewa mtoni.

Hali kadhalika baada ya kufukuliwa, baba wa mtoto, Jackson Makundi aliutambua kutokana na jino moja kukatika, lakini upo ushahidi wa Vinasaba (DNA), uliothibitisha ni wa mwanafunzi huyo.

Kuhusu hoja ya tatu ya kama mwanafunzi huyo alikufa kifo kisicho cha kawaida, mawakili hao wamesema upo ushahidi wa shahidi wa kwanza, Dk Alex Mremi aliyefanya uchunguzi wa kisayansi.

Mawakili hao wameeleza kuwa ripoti ya uchunguzi huo inaonyesha kifo cha mwanafunzi huyo kilisababishwa na kupasuka kwa fuvu kulikosababishwa na kupigwa na kitu ambacho ni butu.

Katika kuiongezea nguvu hoja hiyo, mawakili hao wameegemea ungamo la mshtakiwa Chacha, ambalo anaeleza namna alivyomkimbiza hadi kumpiga kwa panga hadi alipopoteza fahamu.

Kuhusu kama washtakiwa ndio waliomuua mwanafunzi huyo, mawakili hao wameegemea maelezo hayo ya ungamo ambayo yalipokelewa mahakamani kama kielelezo namba P8 cha mashtaka.

Katika maelezo hayo, mshtakiwa alikiri kumuua mwanafunzi huyo na baadaye kuwapigia simu mshtakiwa wa pili, Edward Shayo na wa tatu, Laban ambao walifika hadi eneo la tukio.

Maelezo hayo ambayo ndio msingi wa kesi hiyo, Chacha anaeleza baada ya mshtakiwa wa pili na wa tatu kufika, mshtakiwa wa pili aliwapa maelekezo ya kuubeba mwili huo na kuutupa mtoni.

Kwa mujibu wa mawakili hao, maelezo hayo ya ungamo yanaungwa mkono na ripoti ya mawasiliano ya simu (printout), ambayo ni kielelezo P7 inathibitisha muda ambao washtakiwa waliwasiliana.

Hata hivyo katika majumuisho yake, Wakili David Shillatu anayemtetea Chacha alieleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka hilo bila kuacha mashaka.

Wakili Shillatu katika hoja zake ameeleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuionyesha mahakama uhusiano kati ya mwili ulioopolewa mto Ghona na ule uliofukuliwa makaburi ya Karanga.

Ameeleza kuwa polisi wameshindwa kuionyesha mahakama fomu ya polisi namba 99, ambayo ingethibitisha kuhamishwa kwa mwili kutoka kituo cha Polisi Himo hadi hospitali ya Mawenzi.

Kuhusu maelezo ya ungamo, Wakili huyo alisema maelezo hayo ni batili kwa sababu hayakuchukuliwa kwa kuzingatia sheria na pia mshtakiwa aliyatoa baada ya kufanyiwa mateso ya kiwango cha juu.

Pia ameeleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuleta ushahidi kuonyesha kuwa mshtakiwa wa kwanza kuwa aliwahi kufika Mto Ghona, kwa vile mwenyewe anakana kufika wala kuufahamu.

Kwa upande wake, Wakili Patrick Paul anayemtetea mshtakiwa wa tatu, Laban Nabiswa ameeleza kuwa shahidi wa kwanza wa mashtaka Dk Mremi, unaonyesha Humphrey alikufa Novemba 5, 2017.

Kuhusu maelezo ya ungamo, wakili huyo ameeleza kuwa hakuna mahali mshtakiwa alimtaja mteja wake Laban Nabiswa, kwani katika maeneo yote, anatajwa mtu anaitwa Raban na Mzee Shayo.

Wakili huyo alieleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kujenga ushahidi kuwa mshitakiwa huyo wa tatu alikuwepo eneo la tukio na kielelezo P7 hakikuonyesha mnara wa eneo la tukio ni upi.

Kwa mujibu wa wakili huyo, ameeleza mshtakiwa wa tatu katika utetezi wake alisema waziwazi mahali alipokuwepo usiku huo wa Novemba 6, 2017 kati ya saa 3:00 usiku hadi saa 4:00 usiku.

Mawakili Shillatu na Paul katika hoja zao za majumuisho, wamesisitiza wateja wao hawana hatia na waachiwe huru kwa vile upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shitaka la mauaji ya kukusudia.

Majumuisho ya mwisho kwa mshtakiwa wa pili, Edward Shayo hayakupatikana baada ya wakili wake Elikunda Kipoko kuahidi kulipatia gazeti hili lakini hadi kufikia jana hakufanya hivyo.

Jaji Matogolo alisema pande zote mbili zitajulishwa tarehe ya hukumu kwa njia ya ilani.

Chanzo: mwananchi.co.tz