Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Kiranja mkuu Scolastica asema ‘roll call’ ilifanyika kiholela

56604 Pic+scolastica

Fri, 10 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Aliyekuwa kiranja mkuu wa shule ya Scolastica mwaka 2017, Nicholaus Mabula amesema uhakiki wa wanafunzi siku ya tukio la mauaji ya mwanafunzi Humphrey Makundi ulikuwa ni wa kiholela.

Akitoa ushahidi wake kwa upande wa mshtakiwa wa tatu, Laban Nabiswa, shahidi huyo alidai uhakiki huo (roll call) ulifanywa na Laban na viranja, na hakumbuki kama alimuona Humphrey usiku huo.

Hayo yalijitokeza wakati shahidi huyo akidodoswa na wakili wa Serikali mwandamizi, Abdalah Chavulla baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake kwa kuongozwa na wakili wa Nabiswa, Patrick Paul.

Katika ushahidi wake wa msingi, mshtakiwa alieleza Novemba 6, 2017, mshtakiwa wa kwanza, Hamis Chacha alimpigia simu na kumtaarifu kuwa akiwa nje ya doria amemkurupusha mtu.

Hivyo akamuomba yeye (Laban) aendeshe roll call ili kujiridhisha kama ni mtu wa ndani ama nje ya shule, na alipofanya uhakiki huo kwa kuita jina moja moja, jina la Humphrey liliitika kuwa yupo.

Naye shahidi huyo wa saba ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT) katika Chuo Kikuu Mzumbe, alieleza namna walivyoitisha roll call siku hiyo.

Habari zinazohusiana na hii

Akiongozwa na Wakili Paul, shahidi huyo alisema siku hiyo saa 3 usiku wakati akizungumza na Laban, mshtakiwa huyo wa tatu alipigiwa simu na alimpa mrejesho kuwa ni mlinzi amempigia kuwa kuna mtu amemkurupusha. Alieleza kuwa Laban alimuagiza agonge kengele ili wafanye roll call hiyo na walipoifanya kwa kushirikiana na viranja wenzake watatu, matokeo yalionyesha wanafunzi wote walikuwepo.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake ndipo Wakili Chavulla alipomdodosa kama ifuatavyo:

Wakili Chavulla: Kwa nini mliamua kuitisha roll call kwa wanaume tu?

Shahidi: Ilikuwa ni order (agizo) nililopokea kutoka kwa mwalimu Laban.

Wakili Chavulla: Kwa vile kuna mtu alikurupushwa, busara ilitaka roll call ifanyike kwa wanafunzi wote?

Shahidi: Nakubaliana na wewe.

Wakili Chavulla: Kwa sababu waliitwa wa jinsia moja pekee ilikuwa si sahihi?

Shahidi: Nakubaliana na wewe tulitakiwa tuite jinsia zote.

Wakili Chavulla: Huoni kwamba kwa vile mliita jinsia moja ni kwa sababu ya kujua kwamba ujumbe aliopewa Laban ulikuwa aliyekurupushwa ni mwanamme?

Shahidi: Nakubaliana na hilo. Huenda ile kukurupushwa na mlinzi huyo mtu alikuwa mwanamume.

Wakili Chavulla: Ni sahihi tukisema wanafunzi wenzako walikuwa na desturi ya kuruka ukuta kwenda uraiani?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili Chavulla: Nitakuwa sahihi hata yule Chacha alipomkurupusha mtu yule alikuwa katika majukumu yake ya kuzuia wanafunzi wasiruke ukuta?

Shahidi: Nakubaliana na wewe.

Wakili Chavulla: Wanafunzi hao mliowafanyia roll call walikuwa wangapi?

Shahidi: Ni wanafunzi 470 na zaidi.

Wakili Chavulla: Mlipomuita Huphrey Makundi kwenye ile roll call alikuja mkamuona?

Shahidi: Kuitika kwa Humphrey Makundi sikumbuki ila kuitika jina lingine sio rahisi.

Wakili Chavulla: Humphrey Makundi alipoitwa jina lake hukumuona?

Shahidi: Sikumbuki kama nilimuona au sikumuona.

Wakili Chavulla: Mimi naweza kukuambia mlifanya uhakiki wa wanafunzi kiholela kwa sababu kuna kitu mlichokuwa mnakijua mkaamua kufanya kiholela kufunika kombe, unasemaje?

Shahidi: Kuhusiana kuwa kuna jambo lilikuwa linafichwa hilo silifahamu labda hilo kwamba utaratibu ulifanyika kiholela.

Awali shahidi wa nne wa utetezi, Idd Juma aliiambia mahakama kuwa namba iliyoelezwa kutumiwa Sh500,000 na mshtakiwa wa pili, Edward Shayo, siyo ya Inspekta wa Polisi bali ni namba yake.

Juma, mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoani Kilimanjaro, alisema fedha hizo alitumiwa na mshtakiwa Novemba 7, 2017 kwa ajili ya kusaidia kuhamasisha shughuli za chama hicho.



Chanzo: mwananchi.co.tz