Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Awashushia lawama polisi akidai kuteswa kwa siku tatu

55716 SHAHID+PIC

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Hamis Chacha (31), mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Shule ya Scolastica, amekiri kufanya mawasiliano ya simu na washtakiwa wenzake usiku wa Novemba 6, 2017.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo ambaye ni shahidi wa kwanza wa utetezi alieleza mazungumzo yalijikita kutoa taarifa ya mtu aliyemuona akikurupuka nje ya uzio wa shule na kukimbilia uraiani.

Mwanafunzi huyo, Humphrey Makundi (16) aliyekuwa akisoma kidato cha pili, anadaiwa kuuawa usiku wa siku hiyo na mwili wake kutupwa katika Mto Ghona uliopo umbali wa mita 300 kutoka shuleni.

Chacha ambaye ni mlinzi katika shule hiyo ndiye mshtakiwa nambari moja wakati mshtakiwa wa pili ni mmiliki wa shule, Edward Shayo na wa tatu ni Naban Labiswa ambaye ni mwalimu wa nidhamu.

Mshtakiwa huyo alianza kujitetea juzi saa 9 alasiri mbele ya Jaji Firmin Matogolo wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi na washtakiwa wote watatu kuonekana wana kesi ya kujibu.

Upande wa utetezi unaoongozwa na mawakili Elikunda Kipoko, David Shillatu, Gwakisa Sambo na Patrick Paul unakusudia kuita mashahidi 12 wakiwamo washtakiwa ambao watatetewa na mashahidi tisa.

Habari zinazohusiana na hii

Akiongozwa na Wakili Shillatu kutoa utetezi wake, mshtakiwa huyo ambaye ni mlinzi wa shule hiyo alieleza Novemba 6,2017 aliingia kazini saa 11 jioni na alitakiwa kutoka siku inayofuata saa 12 asubuhi.

Wakati Wakili Shillatu akimuongoza shahidi huyo wa kwanza wa utetezi ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Shillatu: Nini kiliendelea siku hiyo?

Shahidi: Saa 2 usiku nilitoka nje kufanya doria. Nikawa naongea na simu hapo nje.

Wakili Shillatu: Ukiwa hapo nje nini kilitokea?

Shahidi: Ghafla nikasikia mtu anakurupuka anakimbia. Nilimulika lile eneo kwa tochi kama kulikuwa na watu wengine, sikuona.

Wakili Shillatu: Ulifanya nini baada ya kuona mtu amekurupuka

Shahidi: Nilimpigia simu mwalimu mwenzangu Mchamungu (Kiwelu) nikamwambia nilivyotoka nje doria kuna mtu kakurupuka sijafanikiwa kumtambua wala kumfahamu.

Wakili Shillatu: Ulimpigia ili afanye nini?

Shahidi: Nikamwambia naomba uende uwaambie walimu waitishe roll call.

Wakili Shillatu aliiomba mahakama impatie shahidi wake kielelezo namba P7 ambacho ni kumbukumbu ya miamala ya simu (printout) kutoka Vodacom ili ajikumbushe namba na muda wa mawasiliano.

Wakili Shillatu: Huo usiku mtu wa kwanza kuongea naye ni nani?

Shahidi: Mtu wa kwanza kuongea naye alikuwa mke wangu saa 2:57 usiku.

Wakili Shillatu: Baada ya hapo ulimpigia nani mwingine?

Shahidi: Baada ya hapo nilimpigia simu Mchamungu Kiwelu saa 2:59 nikamweleza kuna mtu amekurupuka sijaweza kumtambua.

Wakili Shillatu: Ukamweleza afanye nini?

Shahidi: Nilimwambia aende kuwaambia walimu waitishe roll call ili tujue kama ni mtu wa ndani au wa nje.

Wakili Shillatu: Nani mwingine ulimpigia?

Shahidi: Nilimtafuta mwalimu Laban saa 3:04 usiku nikaongea naye kwa sekunde 5. Mara ya pili nilipiga saa 3:05 usiku nikaongea naye kwa sekunde 4. Niliongea naye tena saa 3:05 kwa sekunde 46.

Wakili Shillatu: Shahidi muda wote huo ulikuwa unamweleza nini mwalim Laban?

Shahidi: Muda wote nilikuwa namweleza kuna mtu amekurupuka ili aitishe roll call.

Wakili Shillatu: Alikujibu nini?

Shahidi: Laban alisema kwa vile yuko shuleni atalifanyia kazi.

Wakili Shillatu: Ulifanya nini tena?

Shahidi: Saa 3:12 usiku niliongea tena na Laban kwa sekunde 18. Nilimuuliza Mchamungu hajakuambia?

Wakili Shillatu: Huyo mtu aliyekurupuka ulimkimbiza hadi wapi?

Shahidi: Huyu mtu aliyekurupuka alikimbilia kuelekea uraiani. Mimi sikumkimbiza.

Wakili Shillatu: Uliwahi kumpigia simu Edward Shayo?

Shahidi: Niliongea pia na Edward Shayo lakini hatukuelewana naye. Nilimpigia baadaye ndio akaniuliza ulikuwa unasemaje nikamwambia nilipotoka nje kuna mtu alikurupuka lakini sikumfahamu.

Wakili Shillatu: Ulivyompa taarifa hiyo akakuambiaje?

Shahidi: Akaniambia nifungulie maji yaingie kwenye ukoka wa shule

Wakili Shillatu: Hiyo namba ya Edward Shayo uliyoongea nayo unaweza kuikumbuka?

Shahidi: Nakumbuka namba ya mwanzo 0754 na ya mwisho 87.

Wakili Shillatu: Mheshimiwa Jaji naomba printout (kumbukumbu za mawasiliano ya simu) kielelezo P7 (Baada ya kupewa na kumpa shahidi aipitie)

Shahidi: Namba hiyo ni (imehifadhiwa) niliongea naye saa 3:07 usiku kwa sekunde 8

Wakili Shillatu: Uliongea naye tena saa ngapi?

Shahidi: Saa 3:08 usiku niliongea naye tena kwa sekunde 6.

Wakili Shillatu: Wewe uliweza kukutana na Edward Shayo?

Shahidi: Sikuweza kukutana na Edward Shayo ila nilikutana na mwalimu Laban akimalizia roll call akaniambia wanafunzi wote wapo hivyo niendelee na shughuli zangu.

Akiendelea kutoa ushahidi wake, shahidi huyo alieleza kuwa Novemba 14,2017 ilifika timu ya polisi ikiongozwa na mkuu wa upelelezi (RCO) wa Mkoa wa Kilimanjaro na maofisa wengine wa polisi.

Siku hiyo, alieleza kuwa polisi walizunguka eneo la shule ndani na nje na baadaye kufanya mahojiano na makundi mbalimbali ukiwamo uongozi wa shule, walinzi, walimu na wanafunzi wa shule hiyo.

Hata hivyo alieleza kuwa Novemba 17, 2017 saa 11 jioni walifika polisi shuleni hapo na kumkamata yeye na Mchamungu Kiwelu kisha wakawapeleka kituo cha polisi Himo na baadaye kituo kikuu cha polisi Moshi.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, akiwa mikononi mwa polisi Novemba 17,2017 hadi Novemba 19, 2017 alifanyiwa mateso makali na askari wakimlazimisha atoe maelezo ya kukiri kosa la mauaji.

Alidai wakati wakimtesa, walimtaka aeleze kuwa Novemba 6, 2017 alimkurupusha mwanafunzi Humphrey Makundi na kumkimbiza, na baadaye kumpiga kwa bapa la panga na baadaye kuanguka.

Akiongozwa na Wakili Shillatu, mshtakiwa huyo alidai polisi walimtaka aseme kuwa baada ya mwanafunzi huyo kuanguka, alipasuka kichwa na yeye aliendelea kumpiga hadi akatulia.

Mshtakiwa huyo alidai katika kueleza hivyo, polisi walimtaka pia aeleze kuwa baada ya mwanafunzi huyo kufa alimpigia mwalimu Laban na baadaye Shayo aliyetoa maelekezo mwili utupwe mtoni.

Alidai kuwa Novemba 20, 2017 polisi walimwambia wanampeleka kwa mtu waliyemsema ni bosi wao na aende kueleza maneno hayo ambayo walitaka ayasema wakati ule wakimfanyia mateso.

Hata hivyo, shahidi huyo hakuweza kufikia mwisho wa kueleza nini kilitokea alipofikishwa kwa bosi huyo baada ya kuelezwa kuwa alikuwa amefunga, hivyo ameanza kusumbuliwa na maradhi ya tumbo.

Jaji aliiahirisha kesi hiyo hadi kesho Jumatatu wakati mshtakiwa atakapoendelea kutoa ushahidi wake huku Jaji akitoa angalizo kuwa muda uliopangwa kwa ajili ya usikilizaji wa kesi unafika ukingoni.



Chanzo: mwananchi.co.tz