Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI YA MWANAFUNZI SCOLASTICA: Mmiliki Scolastica aungana na mlinzi kukata rufaa

62202 Pic+scolastica

Wed, 12 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Washtakiwa wawili katika kesi ya mauaji ya Humphrey Makundi, aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Scolastica wamewasilisha notisi ya kukata rufaa kupinga adhabu walizohukumiwa wiki iliyopita.

Washtakiwa hao ni mmiliki wa shule hiyo, Edward Shayo aliyehukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa kuficha taarifa za mauaji na mlinzi wake, Hamis Chacha aliyehukumiwa adhabu ya kifo.

Hukumu hiyo ilitolewa Juni 3 na Jaji Firmin Matogolo wa Mahakama Kuu. Mbali na Shayo na Chacha, alimhukumu pia Laban Nabiswa kifungo sawa na Shayo.

Hata hivyo, jana wakili wa Chacha, David Shillatu aliwasilisha notisi Mahakama Kuu akiomba kupatiwa nakala ya mwenendo wa kesi hiyo ili aweze kuandaa sababu za rufaa.

“Nimewasilisha ilani ya kukata rufaa kwa ajili ya mteja wangu (Chacha) na nasubiri kupatiwa mwenendo wa shauri hili ili tuweze kwenda hatua ya pili ya kukata rufaa,” alisema.

Wakili Shillatu alisema mteja wake anapinga mambo mawili ambayo ni kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya kukusudia na pia adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa na Jaji Matogolo.

Habari zinazohusiana na hii

Wakati Chacha akiwasilisha notisi hiyo jana, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Frank Mahimbali alisema Shayo pia aliwasilisha notisi hiyo siku moja baada ya hukumu.

“Aliwasilisha notisi hiyo Juni 4 siku moja tu baada ya hukumu na Hamis Chacha naye ameleta. Yule mshtakiwa wa tatu bado,” alisema.

Wakili Patrick Paul aliyemtetea Nabiswa alisema suala la kukata rufaa ni la mteja na bado alikuwa hajapata maelekezo hayo.

Chanzo: mwananchi.co.tz