Moshi. Aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza, Hamis Chacha katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Scolastica, Humphrey Makundi (16), ameamua kukimbilia Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya kifo.
Juni 3, Jaji Firmin Matogolo wa Mahakama Kuu, alimhukumu Chacha kunyongwa hadi kufa, huku washtakiwa wenzake wawili wakihukumiwa kifungo cha miaka minne jela kila mmoja.
Mbali ya Chacha ambaye alikuwa mlinzi wa shule hiyo wengine ni mmiliki wa shule, Edward Shayo maarufu “Kingsize” na mwalimu wa nidhamu wa shuleni hapo, Laban Nabiswa.
Mwanafunzi huyo aliuawa usiku wa Novemba 6, 2017 kwa kupigwa mapanga na Chacha na baadaye akawaita kwa simu Shayo na Nabiswa ambao baada ya kufika, Shayo aliagiza mwili utupwe mtoni.
Akizungumza jana na Mwananchi, wakili aliyekuwa akimtetea Chacha, David Shillatu alisema leo atawasilisha notisi ya kukata rufaa kupinga mambo mawili; hukumu pamoja na adhabu aliyopewa mteja wake.
“Nitawasilisha notisi kesho (leo) kisha nikipewa tu records (kumbukumbu) za Mahakama nitaandaa sababu za rufaa na kuziwasilisha Mahakama ya Rufaa halafu tutasubiri taratibu zingine,” alisema.
Habari zinazohusiana na hii
- MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA :Tafrani yaibuka hukumu mauaji ya mwanafunzi wa Scolastica
- MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Shahidi atoa kielelezo cha panga mahakamani
- MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Mmiliki Scolastica abubujikwa machozi kortini
- MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA : Washtakiwa wana kesi
Wakili Patrick Paul aliyemtetea Nabiswa ambaye ni raia wa Kenya, alisema suala la kukata rufaa ni la mteja na bado alikuwa hajapata maelekezo hayo.