Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAUAJI MWANAFUNZI SCOLASTICA: Baba mzazi wa mwanafunzi aliyeuawa Scolastica afunguka

61701 Scolapic

Sun, 9 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. “Kama si wanafunzi wanaosoma na mwanangu, tusingekaa tujue kuwa mwili ulioopolewa Mto Ghona ulikuwa wa mwanangu. Fununu za mwanangu kuuawa zilijulikana kwa wanafunzi.”

Hayo ni maneno ya Jackson Makundi, ambaye ni baba mzazi wa mwanafunzi Humphrey Makundi (16) wa Shule ya Scolastica aliyeuawa kikatili Novemba 6, 2017 na mwili wake kutupwa Mto Ghona.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi jana, Makundi alisema alitamani washitakiwa wote wahukumiwe kunyongwa, kwa vile hadi sasa, hakuna ushahidi kama wakati wanamtupa mtoni, alikuwa tayari amekufa.

Tayari Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, imemhukumu mlinzi wa shule hiyo,Hamis Chacha adhabu ya kifo, huku mmiliki wa shule, Edward Shayo na mwalimu, Laban Nabiswa wakitupwa jela miaka minne.

Shayo na Laban wamehukumiwa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka minne baada ya Jaji Firmin Matogolo aliyesikiliza kesi hiyo, kuwatia hatiani kwa kosa dogo la kushiriki kosa la jinai kwa kuficha taarifa za mauaji ya Humphrey.

Mahakama imethibitisha kuwa baada ya mlinzi Chacha kumuua mwanafunzi huyo, aliwaita kwa simu wawili hao na kukutana nao eneo la tukio kisha Shayo akatoa maelekezo mwili utupwe Mto Ghona.

Habari zinazohusiana na hii

Maelezo ya ungamo ya Chacha aliyoyatoa kwa mlinzi wa amani akieleza hatua kwa hatua alichokifanya kumuua mwanafunzi huyo, na baadaye kuwaita Shayo na Nabiswa, ndiyo yaliyowakaanga.

Mbali na maelezo hayo, mawasiliano yao ya simu (print out), yalioana na muda uliotajwa katika maelezo ya Chacha kuwa aliwaita Shayo na Nabiswa eneo la tukio baada ya kuua, kisha wakautupa mwili mtoni.

Baba aeleza mwanzo mwisho

Akizungumza jana, Makundi alisema tangu siku ya kwanza alipofika shule na kuzungumza na uongozi wa shule, alitilia mashaka maelezo yao.

“Uongozi wa shule ulisema aliondoka shule tarehe 7.11.2017 lakini kuna wanafunzi wakatofautiana. Wengine walisema tarehe 5.11.2017, wengine 6.11.2017 na wengine 7.11.2017,” alieleza Makundi.

“Lakini kuna wanafunzi wengine nilioongea nao mimi mwenyewe na ndugu yangu anaitwa Ibrahim Kivike wakasema usiku ule mwanangu na wenzake wawili walienda kununua chips.”

Kwa mujibu wa mzazi huyo, wanafunzi hao walitudokeza kuwa wanafunzi wawili walifanikiwa kurejea shuleni, lakini mtoto wake aliendelea kukimbizwa na mlinzi na hakurejea kabisa usiku huo.

“Kauli za wanafunzi zilinifungua akili na kujua kuna jambo limejificha nyuma ya pazia juu ya kutoweka kwa mwanangu. Niliwauliza wakasema wametoa taarifa polisi Himo,” alisema na kuongeza.

“Nilipofika polisi Himo wakaniambia kweli taarifa ya kupotea kwa mwanangu ilitolewa tarehe 10.11.2017. Hapo hapo OCS (mkuu wa kituo) akaniambia kuna mwili uliopolewa Mto Ghona.

“OCS akaniambia huo mwili unaonekana ni wa mtu mzima,” alisema Makundi na kueleza kuwa taarifa hiyo ilizidi kumshtua na kumtia mashaka na kutaka kuuona mwili huo kama anaweza kuutambua.

“Nilishtuka sana kusikia taarifa hiyo kwa vile waliniambia huo mto unapita nyuma ya shule. Nikaambiwa ulipelekwa Mawenzi nikaenda lakini bahati mbaya nikakuta ulizikwa tarehe 12.11.2017 ambayo si siku ya kazi.”

Kulingana na Makundi, aliona kuna mchezo usio wa kawaida kwanini mwili uzikwe haraka kiasi kile hivyo alienda kumuona kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah na mkuu wa upelelezi wa mkoa, Dotto Mdoe.

Alieleza kuwa uchunguzi rasmi wa tukio hilo ulianza na kilipatikana kibali cha mahakama cha kuufukua na ulipofukuliwa aliutambua ni wa mwanae kutokana na alama ya jino moja kukatika.

“Hii kauli ya Mzee Shayo kila wakati kusema kuwa damu ya mtoto wangu haiko kwake au haiko mikononi mwake ni kauli inayoumiza sana. Yaani ushiriki kumtupa mtoto halafu useme haiko kwako?” Alihoji.

“Tangu day one (siku ya kwanza) nilipofika shuleni nilihisi Mzee Shayo anajua kitu. Moyo wangu ulikuwa mzito sana juu yake hasa baada ya wanafunzi kutudokeza juu ya tukio la usiku wa tarehe 6.11.2017”.

“Nilitegemea Mzee Shayo baada ya kuitwa pale na Chacha angeamuru mtoto wangu apelekwe hospitali pengine angepona. Lakini yeye anaagiza atupwe mtoni halafu unasema damu haiko kwako.”

Amshukuru Jaji, Polisi na wanasheria

Baba huyo mzazi aliishukuru Serikali ya Rais John Magufuli kwa jinsi anavyoisimamia Serikali, akaishukuru pia Mahakama kwa kusikiliza kesi hiyo kwa weledi kwani mwisho wa siku haki imetendeka kwa wahusika.

“Kulikuwa na mizengwe mingi ilizunguka hii kesi kule mwanzo ikabidi nimwandikie barua Jaji Kiongozi na kweli aliyafanyia kazi malalamiko na kumteua Jaji Matogolo aisikilize,”alieleza Makundi.

Alitumia fursa hiyo, kumshukuru Jaji Matogolo kwa namna alivyosikiliza shauri hilo kwa weledi mkubwa na kufikia maamuzi ya haki, akisema pamoja na sheria lakini Mungu alikuwa katikati yake.

Pia alimpongeza Wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande na wale alioshirikiana nao kuendesha kesi hiyo akisema waliiendesha kwa weledi ambao umeisaidia mahakama kufikia maamuzi ya haki.

Halikadhalika aliwapongeza baadhi ya polisi waliopeleleza tukio hilo kwa weledi, akisema polisi wachache wa kituo cha Himo waliojaribu kuvuruga upelelezi wanapaswa kuona aibu.

Hizi ndizo adhabu alizotoa Jaji

Akisoma adhabu baada ya kuchambua ushahidi na kuzingatia maombolezo ya washitakiwa, Jaji Matogolo alisema kosa la mauaji ya kukusudia kwa mujibu wa sheria ni moja nayo ni adhabu ya kifo.

“Kwa mshitakiwa wa kwanza (Chacha) adhabu iliyowekwa kwa mujibu wa sheria ni moja tu nayo ni kifo. Kwa hiyo utanyongwa hadi ufe. Nimefungwa mikono siwezi toa adhabu mbadala,” alisema Jaji.

Kuhusu mshitakiwa Shayo maarufu kama Kingsize na Nabiswa, Jaji Matogolo alisema wao walipaswa kushiriki kulea watoto, lakini wakashiriki kuficha taarifa za mauaji ya mwanafunzi wao, Humphrey.

“Nimesikiliza maombolezo yaliyotolewa na mawakili wenu pamoja na nyinyi wenyewe lakini adhabu ndogo hutolewa kulingana na kosa na adhabu hiyo ilenge kumrekebisha mhalifu,”alisema Jaji.

Jaji Matogolo alieleza katika hukumu yake hiyo kuwa adhabu hiyo pamoja na kumrekebisha mhalifu, lakini lazima ifinye ili kutoa funzo kwa mhalifu na jamii ili isifikirie kutenda kosa kama hilo.

Chanzo: mwananchi.co.tz