Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAITI ILIYOKUTWA KWENYE BEGI:Mawakili waomba kesi isikilizwe upya

15890 Maiti+pic TanzaniaWeb

Thu, 6 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Miaka saba baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa raia wa India, Vinoth Nadhesan Praveen, wakili wake ameomba kesi hiyo isikilizwe upya.

Raia huyo wa India alitiwa hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia rafiki yake, Abdul Abdallah.

Wakati Praveen akisubiri hatima ya rufaa yake aliyoikata Mahakama ya Rufani akipinga hukumu hiyo, wakili wake, Melkiory Sanga ameiomba mahakama iamuru kesi hiyo irudishwe Mahakama Kuu ianze upya.

Praveen alihukumiwa adhabu hiyo mwaka 2011 na Jaji Dk Fauz Twaib, kwa kosa la kuua alilolifanya Februari 6, 2009, kisha akauweka mwili huo kwenye begi la nguo na kwenda kuutelekeza ndani ya gari kwenye maegesho ya jengo la JM Mall.

Licha ya kukubali kutenda kosa hilo wakati wa utetezi wake, hata hivyo Praveen hakukubaliana na hukumu na adhabu hiyo badala yake alikata rufaa. Rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa jana na jopo la majaji watatu; Augustine Mwarija, Sivangilwa Mwangesi na Stella Mugasha, lakini kabla ya kuanza kusikiliza hoja za rufaa, Jaji Mwarija aliibua hoja ya kasoro katika mwenendo wa kesi hiyo Mahakama Kuu.

“Kabla ya kuendelea tunaomba maoni yenu kuhusu joint opinion (maoni ya pamoja) ya court assessors (washauri wa mahakama) kama ilikuwa na athari zozote katika uendeshaji wa kesi,” alisema.

Baada ya kupewa nafasi hiyo mawakili wa pande zote walikiri kilichofanywa na washauri hao wa mahakama ni kinyume cha sheria, kwani sheria inaelekeza kila mshauri atoe maoni yake mwenyewe kwa mdomo na mahakama iyaandike.

Wakili wa Serikali, Cecilia Mkonongo na Sanga anayemwakilisha mrufani, walikiri kwamba kutokana na kasoro hiyo mwenendo wa kesi hiyo kuwa batili.

Hata hivyo, walitofautiana namna ya kurekebisha kasoro hiyo wakati Mkonongo aliiomba mahakama hiyo iamuru kesi hiyo irudishwe Mahakama Kuu isikilizwe upya kuanzia sehemu ya washauri kutoa maoni yao mmoja mmoja, Sanga aliomba isikilizwe upya kuanzia mwanzo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mahakama iliahirisha shauri hilo kwa ajili ya kuandaa uamuzi wa ama kesi hiyo irudishwe Mahakama Kuu kusikilizwa upya kuanzia sehemu ya maoni ya washauri wa mahakama, au ianze upya kuanzia shahidi wa kwanza.

Chanzo: mwananchi.co.tz