Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lugola amsweka mahabusu mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Mtwara

14240 Lugola+pic TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Wakati taarifa ya Wizara ya Ndani ikieleza kuwa mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Mtwara (OCS), Ibrahim Mhando amewekwa mahabusu kwa amri ya waziri, kamanda wa polisi wa mkoa huo, Lucas Mkondya amesema hana taarifa ya agizo hilo.

Taarifa iliyotolewa na wizara jana ilieleza kuwa Mhando aliwekwa mahabusu kwa amri ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kwa kile kilichoelezwa kuwa ameshindwa kuwaweka mahabusu watuhumiwa wanne.

Miongoni mwa watuhumiwa hao ni mhandisi mshauri wa kampuni ya Y&P Architects, Benjamin Kasiga ambaye anadaiwa kutoa taarifa ya uongo kwa waziri huyo kuhusu ujenzi wa ofisi ya Uhamiaji mkoani humo.

Hata hivyo, Mkondya alipotafutwa kwa simu jana kujua iwapo OCS bado yupo ndani, alisema hana taarifa za agizo la waziri.

Hata alipoelezwa kuwa taarifa ya wizara inaonyesha naye alikuwapo, Mkondya aliendelea kusisitiza kuwa hafahamu.

Tukio hilo lilitokea jana asubuhi wakati Lugola na katibu mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu walipofika katika kituo hicho kwa kushtukiza.

Lugola alipokuwa anakwenda uwanja wa ndege wa Mtwara kwa ajili ya kurudi jijini Dar es Salaam, ghafla aliamuru msafara kwenda Kituo Kikuu cha Polisi ili athibitishe iwapo mtuhumiwa ambaye alielekeza juzi usiku akamatwe na kuwekwa mahabusu kama polisi walitekeleza agizo lake.

Hata hivyo, Lugola baada ya kufika kituoni hapo alimkuta mtuhumiwa huyo akiwa chumba cha upelelezi badala ya kuwekwa mahabusu, hivyo akamuuliza kamanda Mkondya sababu za kutotekelezwa amri yake.

“Hivi ndivyo polisi mnafanya hivi, haya ndiyo madudu mnayoyafanya? Tabia hii siku zote tunaipinga inachafua Polisi na hii ndiyo tabia yenu. Najua ndiyo maana nimekuja ghafla, mnafahamu maadili ya Jeshi?

“RPC hawa polisi wako wanafanya nini? OCS njoo hapa, kwa nini umeweka hawa watuhumiwa chumba cha upepelezi badala ya mahabusu, nawe unaingia ndani kwa kushindwa kuwaweka ndani hawa watuhumiwa, RPC muweke ndani sasa hivi huyu,” aliamuru.

Hata hivyo, Mkondya alimweleza Lugola kuwa askari hao walifanya makosa kwa kutowaweka mahabusu watuhumiwa hao.

Akijitetea kabla ya kuwekwa mahabusu pamoja na watuhumiwa ambao alishindwa kuwaweka mahabusu, Mhando alisema sababu kubwa chumba kilijaa na huwa wanafanya hivyo mara chache inapotokea.

Hata hivyo, Lugola aliipinga kauli hiyo kuhusu mahabusu hiyo kujaa wakati nafasi ya kukaa watuhumiwa hao ilikuwapo.

“Mbona nafasi ipo pale mahabusu, ile pale nafasi naiona, siwezi kukubaliana na uzembe huu na hii ni tabia yenu huwa mnakamata watuhumiwa lakini baadhi hamuwaweki mahabusu, unanidanganya kuwa mahabusu imejaa, hii haikubaliki!” alisema Lugola.

Chanzo: mwananchi.co.tz