Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishina msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo, amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa kukamata watuhumiwa (47) ambao walikamatwa na jumla ya lita 4000 za pombe haramu aina ya gongo (moshi).
ACP Masejo ameeleza hayo leo wakati akitoa taarifa kwa wanahabari, ambapo amesema kati yao watuhumiwa nane (08) wamefikishwa mahakamani, na kuhukumiwa kwenda jela vifungo mbalimbali hadi mwaka mmoja na kesi nyingine zipo kwenye mchakato.
Ameendelea kusemea katika kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa kukamata bunda 3500 za Dawa za kulevya aina bhangi pamoja na mirungi.
Kamanda Masejo amesema Watuhumiwa wote hao walikamatwa katika maeneo tofauti tofauti ndani ya halmashauri ya wilaya ya Karatu, ambapo watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika hatua nyingine kamanda Masejo ameviambia vyombo vya habari kuwa Jeshi la Polisi liliendesha operesheni ya wiki moja, na kuwakamata madereva wanaovunja sheria za usalama barabarani kumi na tatu (13).