Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu azidi kukwamisha kesi yake ya uchochezi

72532 Pic+lissu

Thu, 22 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kesi ya Uchochezi inayomkabili  aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na wenzake watatu imekwama kusikilizwa kutokana na mwanasheria mkuu huyo wa Chadema kuwa nje ya nchi kwa matibabu.

Mbali na Lissu washtakiwa wengine ni Mhariri wa Gazeti la Mawio,  Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi.

Kesi hiyo kila inapotajwa mahakamani inaahirishwa kutokana na Lissu kutokuwepo nchini.

Leo Alhamisi Agosti 22, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakili wa Serikali, Sylivia Mitando amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa na mshtakiwa  bado hajarudi nchini hivyo aliiomba Mahakama hiyo ipange tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo hakimu Simba ameahirisha shauri hilo hadi Septemba 23, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na sheria ya magazeti ya mwaka 2002.

Habari zinazohusiana na hii

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam washtakiwa , Jabir, Mkina na Lissu waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo manispaa ya Ilala alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa msajili wa magazeti.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz