Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lema kushtakiwa Kenya

Addffbb3351eadb1fb8ee9b230123b17 Lema kushtakiwa Kenya

Tue, 10 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe amesema aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema alitarajiwa kupandishwa kizimbani nchini Kenya kujibu mashitaka ya kuingia nchini humo bila kibali.

Mwaisumbe alisema jana kwa njia ya simu kuwa hadi jana Lema alikuwa Kenya ila hakuwa na taarifa kama ni kweli mwanasiasa huyo alisomewa mashitaka.

Alisema Lema alikamatwa nchini Kenya baada ya kuingia huko kupita njia za panya. Alisema wakati Lema anakamatwa gari lililokuwa limbebe likikuwa linamsubiri upande wa Kenya.

Alisema mbunge huyo wa zamani wa Arusha Mjini kwa miaka 10, alizuiwa kuingia Kenya kwa kuwa hakuwa na vibali au nyaraka halali za kuingia nchini humo na baada ya kuona amezuiwa juzi alipita njia za panya.

“Tuliwasiliana na askari kanzu wa Kenya na baada ya kuwaeleza waliweka mitego yao na kumkamata huko Kenya,” alisema Mwaisumbe ambaye wilaya yake inapakana na Kenya kupitia Mpaka wa Namanga.

Msemaji wa Idara ya Uhamiaji Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Mrakibu wa Uhamiaji, Paul Mselle alisema jana kuwa idara hiyo haina taarifa rasmi ya kukamatwa Lema na familia yake.

Mselle alisema kwa njia ya simu kuwa habari za kukamatwa kwa Lema amezisikia kupitia mitandao ya kijamii.

“Kama Lema kakamatwa amekamatiwa nje ya nchi, sisi hatuna taarifa hizo hadi sasa tunafuatilia na tukikabidhiwa nchini kwetu tutasema ila hadi sasa hatuna hizo taarifa zaidi ya kuzisikia kupitia mitandao ya kijamii maana kakamatwa nje ya nchi,” alisema Mselle.

Lema alishindwa na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mrisho Gambo katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Lema na mkewe, Neema Godbless na watoto wao watatu, Allbless, Brilluance na Terrence wanadaiwa kukamatwa katika Kaunti ya Kajiado nchini Kenya baada ya kuvuka mpaka kuingia nchini humo.

Katika hatua nyingine, DC Mwaisumbe alisema jana kuwa aliyekuwa mgombea ubunge Singida Kaskazini (Chadema), Lazaro Nyalandu juzi alizuiwa kuingia Kenya kupitia mpaka wa Namanga kwa sababu hakuwa na nyaraka muhimu.

Alisema Nyalandu alikuwa na gari ambalo halikuwa na usajili na walimuamuru apeleke nyaraka hizo za gari hilo na asipofanya hivyo atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Chanzo: habarileo.co.tz