Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lambalamba 170 wakamatwa Rukwa

Lambalamba 170 Wakamatwa Rukwa Lambalamba 170 wakamatwa Rukwa

Mon, 21 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi mkoani Rukwa limewakamata waganga wa kienyeji 170 maarufu kwa jina la lambalamba wakiwamo wanawake 37 wanaotuhumiwa kujishirikisha na ramli chonganishi.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwalaghai wananchi kuwa wana uwezo wa kuwatambua na kuwaadhibu wachawi, kusafisha nyota na kufufua wafu hivyo kusababisha chuki, husuda, na taharuki.

Inadaiwa kuwa lambalamba ‘wamevamia’ Mkoa wa Rukwa wakitoka mikoa ya Lindi, Morogoro, Kigoma na nchi jirani ya Zambia. Huwatoza wananchi hadi Sh milioni 10 yakiwa ni malipo ya huduma ya kuondoa uchawi kwenye nyumba na kuwatambuwa wachawi na kuwaadhibu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa,Theophista Mallya alilieleza HabariLEO kuwa waliwakamata ‘lambalamba’ katika msako uliofanyika katika vijiji 17 vilivyopo katika wilaya za Kalambo na Nkasi.

Alisema lambalamba 95, wanaume wakiwa 61 na wanawake 34, walikamatwa wilayani Nkasi. Walikamatwa katika vijiji vya Kabwe, Kipili, Miovu, Nkana, Wampembe na King’ombe vilivyopo wilayani Nkasi.

Wilayani Kalambo walikamatwa 75 ambao kati yao, 72 ni wanaume na wanawake watatu waliokamatwa katika vijiji vya Zyangoma, Serengoma, Kilesha , Kasanga, Kapozwa, Mpombwe na Samazi

Kamanda Mallya alisema katika msako huo pia vifaa vilikamatwa vikidaiwa kutumiwa na watuhumiwa hao. Navyo ni vinyago,vibuyu, tunguli, dawa za miti shamba, vipaza sauti na ngozi za wanyamapori.

“Inadaiwa kuwa lambalamba anapoingia ndani ya nyumba anakuwa ameshikilia kioo ambacho kinadaiwa kuwa na ‘sensor’ (utambuzi) inayotambua kama kuna uchawi au mchawi ndani ya nyumba,” alisema.

Aliongeza “Mbaya zaidi wananchi kwa hiyari yao wenyewe wanawapatia wasichana wenye umri mdogo kufanya nao mapenzi huku wanaume wengine wakiwa radhi lambalamba kufanya mapenzi na wake zao”.

Mallya aliomba viongozi wa dini waendelee kuwaombea na kuwaelimisha waumini wao ili wawakomboe kutoka kwenye kuamini lambalamba.

Alisema wengi wa waganga hao, wanahifadhiwa katika vijiji na visiwa vilivyo katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika wilaya za Nkasi na Kalambo ambavyo havifikiki kwa urahisi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live