Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Laini ya simu ilivyowakamatisha wauaji wa dereva bajaji

Laini Za Simu Zisizohakikiwa Kuzimwa Januari 31, 2023 Laini ya simu ilivyowakamatisha wauaji wa dereva bajaji

Sun, 21 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maduhu Dwisha, dereva wa bajaji, aliondoka nyumbani asubuhi na mapema, akimuaga mkewe, Mwadawa Ally kuwa anakwenda kwenye mihangaiko, siku inayofuata maiti yake ilipatikana kwenye kalavati.

Maiti yake iligunduliwa na watoto waliokuwa wanapita wakitoka shuleni, ambao waliona damu nyingi kwenye kalavati lililopo  barabara kuu ya Igunga-Kahama, wakamwendea trafiki na kumweleza walichoona, kumbe ni mwili wa Maduhu.

Pikipiki ya magurudumu matatu aliyokuwa akiitumia kibiashara ikawa haijulikani ilipo, lakini Waswahili wanasema damu ya mtu huwa haipotei, kwani hakuna aliyejua kuwa laini ya simu ya marehemu iliyochukuliwa na wauaji, ndiyo ingewafanya wakamatwe ‘kama kuku.’

Hii ndiyo simulizi ya mauaji ya Maduhu aliyekuwa anafanya shughuli zake katika mji wa Igunga mkoani Tabora, akiwa ndiyo kwanza amenunua bajaji mpya, wauaji wakajifanya wateja; wakamkodi, kumuua na kumpora bajaji hiyo.

Mauaji hayo yalitokea Machi 2, 2017 na uchunguzi uliofanywa na makachero wa Polisi, uliwezesha kuwakamata Safari Mtelemko, Safari Kija na Emmanuel John, ambaye alifariki dunia aliporuka kwenye gari la polisi.

Safari Mtelemko na Safari Kija walifunguliwa mashtaka ya mauaji ya kukusudia. Julai 2, 2021, Jaji Amour Khamis aliwatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kifo, wakakata rufaa lakini Mahakama ya Rufani ilibariki adhabu hiyo mwaka 2023.

Katika hukumu ya Oktoba 23, 2023 ambayo nakala yake imepatikana jana Januari 20, 2024 katika mtandao wa mahakama, Jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye, Zephrine Galeba na Benhaji Masoud, wanasisitiza wawili hao waendelee na adhabu hiyo.

Majaji hao katika rufaa hiyo wamesema ingawa wamefuta ushahidi wa vielelezo vinne ambavyo ni maelezo ya onyo na yaliyotolewa kwa mlinzi wa amani ya kila mshtakiwa kwenye mwenendo wa kesi, lakini ushahidi uliobakia unathibitisha shitaka bila kuacha shaka.

“Tunaona kuwa ushahidi uliobaki kwenye rekodi baada ya kutupilia mbali vielelezo P19, P20, P21 na P22 (maelezo) unathibitisha bila shaka yoyote, kwamba waombaji walimuua Maduhu au walishiriki katika mauaji hayo,” wamesema majaji katika hukumu.

Ilivyokuwa siku ya mauaji

Machi 2, 2017, Maduhu aliondoka nyumbani na bajaji yake mpya kwenda kutafuta riziki, lakini hakurejea jioni kama ilivyokuwa kawaida na utaratibu wake wa maisha.

Hadi asubuhi ya siku iliyofuata, haikujulikana alipo Maduhu Dwisha wala bajaji yake. Ilipofika saa tano asubuhi, mkewe Mwadawa Ally, alienda Kituo cha Polisi Igunga kutoa taarifa ya kutowekwa kwa mumewe.

Kituoni alipokewa na askari ambao walimpatia taarifa hiyo Paschal Hosea, aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa wilaya (OC-CID) Igunga. Mwadawa aliwapa askari namba ya simu ambayo alikuwa Maduhu akiitumia.

Pia aliwapa taarifa ya bajaji ya mume wake namba MC 554 BPC aina ya TVS, rangi ya bluu na akawaambia kuwa muda wote hutembea na pochi nyeusi mfukoni, yenye maandishi Lacost’ ikiwa na nembo ya mamba.

Kutokana na taarifa hizo, uchunguzi na msako wa kumtafuta Maduhu Dwisha ulianza, lengo likiwa ni kumpata akiwa hai au mfu.

Wakati msako ukiendelea, trafiki aitwaye WP Neema alikuwa kazini katika barabara kuu ya Igunga - Sikonge - Singida.

Akiwa hapo, watoto wa shule ya msingi waliokuwa wanapita walimfuata na kumjulisha askari huyo kuwa wameona damu imesambaa kwenye kalavati, walimchukua kumpeleka hapo, alipofika aliona mwili wa binadamu.

Trafiki alimjulisha OC-CID ambaye alifika na timu yake, pamoja na madereva wa bajaji. Katika eneo ulipokuwa mwili huo, madereva wa bajaji waliutambua kuwa ni wa wenzao, ulichukuliwa na kupelekwa mochwari.

Uchunguzi wa mwili wa marehemu uliofanywa na Dk Sange Saadallah wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga ulibaini chanzo cha kifo ni kutikiswa kwa ubongo na kukosa hewa. Aliwasilisha ripoti yake kama kielelezo P4.

Laini ya simu yawaponza wauaji

Makachero wa Polisi wakiongozwa na OC-CID, walienda ofisi za Vodacom ambako walipata ripoti ya mawasiliano ya simu ya Maduhu ikionyesha aliyekuwa na simu yake Machi 2, 2017 alikuwa Igunga na Nzega.

Siku iliyofuata, Machi 3, 2017, simu hiyo ilionekana ikitumika Kahama, Mkoa wa Shinyanga. OC-CID alituma timu ya makachero hadi Kahama kumtafuta mtu aliyekuwa akitumia simu ya Maduhu.

Timu hiyo ilifika Kahama Machi 16, 2017, siku iliyofuata ilikaa na kupitia kwa umakini ripoti ya mawasiliano na kuamua kuwasiliana na kitengo cha makosa ya kimtandao Dar es Salaam ili kupata namba zinazowasiliana nayo.

Walipewa namba tatu, moja ilipopigwa alipokea mwanamke, hivyo makachero wakatumia mbinu ya kumghilibu kuwa kuna mzigo wake, akakubali kukutana na ofisa aliyempigia. Walipokutana akajitambulisha anaitwa Glory.

Alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Kahama, huko aliambiwa aipige namba ya Maduhu. Alipoipiga likatokea jina la Safari, alipoulizwa ni nani akasema ni dereva bajaji ambaye anamtumia mara kwa mara katika mizunguko yake.

Akaambiwa ampigie, akampigia kumwambia amfuate soko la mazao kwa sababu kuna vitu amenunua, hivyo anataka kuvipeleka nyumbani.

Dereva huyo wa bajaji aliwasili saa 11.00 jioni na bajaji, alikamatwa na kupelekwa polisi Kahama.

Mtuhumiwa afunguka kila kitu

Akiwa Kituo cha Polisi Kahama, mtuhumiwa huyo alijitambulisha anaitwa Safari Kija Elikana na kuwathibitishia polisi kuwa anafahamu namba ya Maduhu, lakini iliingizwa kwenye simu yake na mwenzake, Safari Anthony Mtelemko.

Polisi walimtaka ampigie simu huyo Mtelemko, alimpigia na kumwambia amekamatwa na trafiki, hivyo anaomba aende kumsaidia Sh30,000 za faini, akamwambia yuko ‘car wash’ anaosha bajaji, akaahidi kumpa msaada huo mara tu atakapomaliza kazi hiyo.

Baada ya muda mfupi, Mtelemko alifika polisi, naye akakamatwa. Katika mahojiano ya awali aliiambia timu ya uchunguzi kuwa alishiriki tukio la Igunga na kwamba katika matukio mengine, kila wakiiba bajaji wanamuua dereva.

Aliwaeleza polisi kuwa bajaji waliyoiba siku za karibuni alikuwa nayo akiiosha kwenye kituo cha kuuzia mafuta cha Usagali.

Aliwapeleka polisi, huko walikuta bajaji ya bluu aina ya TVS yenye namba za usajili MC 554 BPC.

Mtelemko alikiri kwa polisi kuwa waliipata bajaji hiyo Igunga Darajani, ambako walimuua dereva.

Pia alieleza kuwa waliiba bajaji hiyo na walichukua simu iliyokuwa mfukoni mwa marehemu. Alieleza walishirikiana na Safari Kija Elikana.

Vitu vya marehemu vilivyonaswa

Timu ya makachero wakiwa na Mtelemko, walikwenda nyumbani kwake eneo la Nyasubi, Kahama kufanya upekuzi. Walipoingia chumbani wakiongozwa na Mtelemko, walifunua godoro wakakuta vitu mbalimbali.

Miongoni mwa hivyo ni magurudumu matatu ya bajaji, mfuko wa nailoni ukiwa na vipuri vya bajaji, pochi nyeusi ikiwa na maandishi lacosta, picha (passport size) na kitambulisho cha mpigakura, vyote vya marehemu Maduhu.

Wakiwa hapo, Mtelemko aliwakabidhi polisi simu ya marehemu ambayo alikuwa nayo mfukoni.

Vyote vilipelekwa polisi na wao walibaki na Mtelemko Kahama ili kuendelea kuwasaka watuhumiwa wengine walio katika mtandao huo.

Mtelemko alipohojiwa na polisi kuhusu washirika wengine, aliwataja Emmanuel John na Yasin Abdu. Alisaidia kukamatwa kwa Emmanuel, ambaye alikufa baadaye lakini Yasin hajawahi kukamatwa hadi leo.

Kwa mujibu wa polisi, Emmanuel John aliruka kwenye gari la polisi lililokuwa kwenye mwendo, wakati wanatoka Nzega kwenda Igunga kumkamata Yassin Abdu, lakini watuhumiwa hao wawili walidai aliuawa na polisi Igunga wakati wanamtesa.

Walilenga bajaji mpya

Kwa mujibu wa hukumu na maelezo ya ushahidi, Safari Elikana aliwaeleza mashahidi wawili, wa 4 na wa 5 ambao ni maofisa polisi kuwa Emmanuel na Yasin Abdu jukumu lao lilikuwa kwenda Igunga kutafuta madereva wenye bajaji mpya.

Wakishalenga bajaji wanayoitaka, watajitahidi kujenga urafiki na dereva kwa kumwaminisha kuwa wao ni wateja waaminifu, baadaye watamwita Safari na Mtelemko waende Igunga kwa ajili ya kutekeleza uporaji na mauaji.

Baada ya kupokea wito, Safari Elikana na Mtelemko watakwenda Igunga mchana na wanapofika kituo cha mabasi Igunga, Emmanuel John na Yassin Abdu watamwita dereva bajaji waliyemlenga ili akawasaidie kuwachukua wageni wao.

Dereva atapewa maelekezo kuwa akishawachukua wageni hao, awapeleke mahali ambako Emmanuel John na Yassin Abdu wanasubiria na kwa kawaida, huwa ni kwenye barabara kuu ya Igunga-Kahama, umbali wa kilomita tatu kutoka mjini.

Baada ya dereva kufika eneo hilo, Safari Kija na Safari Mtelemko watamkaba na kumnyonga kwa kutumia kamba na kumfanya akose pumzi, na mzunguko wa damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye ubongo kusimama na kufariki dunia.

Katika kipindi cha purukushani, Emmanuel John na Yasin Abdu watajitokeza kuongeza nguvu ili mauaji yafanyike katika muda mfupi kadri iwezekanavyo.

Hapo wauaji hao wanne watachukua mwili wa dereva bajaji na kuuweka nyuma ya bajaji na kwenda kwa mwendo kasi kuelekea Nzega, ambako wanautupa vichakani katika kijiji cha Igogo na kuendelea na safari na bajaji hadi Kahama mjini.

Walivyojitetea kortini

Katika utetezi, washtakiwa Safari Kija na Safari Mtelemko walikana kutenda kosa la mauaji na kueleza namna walivyokamatwa kwa tarehe tofauti.

Safari Mtelemko alieleza  alikamatwa Machi 18,2017 akiwa njiani kwenda Kahama akitokea Nhongolo, wakati Safari Kija alisema alikamatwa na Polisi Machi 17,2017 katika mtaa wa CDT wilayani Kahama.

Walieleza baada ya kukamatwa, walipelekwa Kituo cha Polisi Kahama na Machi 18, 2017 wakiwa kituoni na hawajuani, waliunganishwa na Emannuel John wakitakiwa kukiri kwamba wanafahamiana na walishiriki mauaji.

Walipokataa kukiri walidai waliteswa na Machi 18, 2017 saa 10 jioni, walipelekwa Kituo cha Polisi Igunga, ambako walidai walipewa mateso makali.

Walidai mateso yalisababisha kifo cha mwenzao. Walijitetea hawakuwahi kukiri kufahamiana wala kushiriki mauaji. Hilo liliulazimisha upande wa mashtaka kuita mashahidi 14 na kuwasilisha vielelezo 22.

Miongoni mwa mashahidi, wanane walikuwa maofisa wa polisi wenye vyeo na utalaalamu mbalimbali, wakiwamo wa kitengo cha makosa ya mtandao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live