Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

LHRC yajitosa sakata la kijana aliyepigwa risasi na mwajiri wake Morogoro

RISASI 2222222222 LHRC yajitosa sakata la kijana aliyepigwa risasi na mwajiri wake Morogoro

Thu, 19 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku mbili baada ya sintofahamu ya kijana aliyepigwa risasi na mwajiri wake mkoani Morogoro kuripotiwa na gazeti hili, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeingia kati kuhakikisha haki inatendeka.

Hivi karibuni iliripotiwa kuhusu tukio la kijana, Benjamin Shinda (26), mkazi wa Mtibwa, Morogoro aliyepigwa risasi na mwajiri wake Januari 12, akiendelea kutaabika hospitali, mtuhumiwa alikuwa huru uraiani.

LHRC kupitia kwa Mkurugenzi wake, Anna Henga aliiambia Mwananchi jana baada ya kuona taarifa hiyo wamelazimika kumtuma mtetezi wa haki za binadamu,  aliyeko mkoani Morogoro kufuatilia kwa karibu.

“Tumemtuma mtetezi wetu wa haki za binadamu aliyepo Morogoro anafuatilia kwa karibu, kwa sababu ni jambo baya,” alisema.

Kinachoshangaza, alisema ni mtuhumiwa kutokamatwa hadi sasa kama ilivyoelezwa kwenye taarifa.

“Tunataka tujue kwa nini hajakamatwa, tunajua kesi hii inadhaminika, lakini angalau akamatwe taratibu zifanyike mahakamani itajulikana kama ana hatia au laa,” alisema.

Akizungumza kuhusu hali yake, Shinda alisema Januari 15, mwaka huu aliruhusiwa kutoka hospitalini baada ya madaktari kumpa huduma zote, ikiwemo kutoa risasi na kusafisha majeraha.

Hata hivyo, alibainisha kwa sasa hali yake imebadilika na kuwa mbaya zaidi kwani mguu umevimba, anapata maumivu makali na ganzi.

“Kesho (leo) natarajia kurudi hospitali hali yangu sio nzuri, mguu umevimba kupitiliza nasikia maumivu makali nyakati za usiku na muda mwingine nahisi ganzi,” alieleza.

Alipoulizwa iwapo kuna taarifa zozote kuhusu mtuhumiwa, alisema hajui lolote zaidi ya kile alichojibiwa na polisi kwamba hatua zinaendelea kuchukuliwa.

Akizungumzia suala hilo,  mjomba wake, Emmanuel Siame alisema baada ya mgonjwa kutolewa hospitali, yeye aliongozana na askari polisi kwenda kuchukua picha za mionzi (X-Ray) na risasi zilizotolewa.

“Nilitakiwa kwenda na polisi katika hospitali aliyotibiwa mgonjwa, walipofika pale waliomba wapewe picha za X-Ray na risasi zilizotolewa na walipewa wakasema wanaendelea na uchunguzi,” alisema.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mukama alitaka mazungumzo yakafanyike ofisini kwake.

“Siwezi kuzungumza hapa maana kwenye simu mtu anajitambulisha vyovyote vile, njoo ofisini tutaongea,” alisema. Hata hivyo, mwandishi alipofika ofisini kwake saa 11 jioni hakuwepo.

Lilivyotokea

Siku nne kabla ya tukio Shinda aliajiriwa na Mzee Mashelle kuwa dereva wa trekta,  ambalo lilishindwa kufanya kazi kutokana na ubovu.

Hali hiyo ilisababisha mwajiri huyo kumtuhumu Shinda kuwa anamwibia fedha za kazi na si kwamba trekta lake bovu, kama anavyomweleza.

Kutokana na hilo, Mzee Mashelle alimpiga risasi kijana huyo akimtaka amweleze iwapo anamwibia ama laa,  na baada ya kutekeleza tukio hilo alimpa Sh20,000 akatibiwe katika duka la dawa.

Awali, jeshi la polisi wilayani Mvomero licha ya kueleza hakukuwa na mtuhumiwa aliyeshikiliwa kwa tuhuma hizo kituoni hapo, lilielekeza atafutwe kamanda wa polisi mkoa kwa maelezo zaidi, ambaye pia alidai ndiyo kwanza alikuwa anahamia hivyo hafahamu lolote kuhusiano na tukio hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live