Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa kina kuhusu hoja sita kesi ya Bandari

BANDARIII Kwa kina kuhusu hoja sita kesi ya Bandari

Thu, 27 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imetaka kufahamu kama kilichosainiwa katika makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii, kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai kuhusu uwekezaji katika bandari nchini ni mkataba au la.

Mahakama hiyo ilihoji swali hilo jana, wakati mawakili wa pande mbili katika kesi ya kupinga makubaliano hayo walipowasilisha mambo matano waliyoafikiana kuwa ndiyo kiini cha kesi, ambayo wanaitaka Mahakama hiyo kuyatolea uamuzi.

Miongoni mwa mambo hayo, ni iwapo waliosaini makubaliano hayo walikuwa na nguvu za kisheria kufanya hivyo.

Baada ya kuwasilisha suala hilo, ndipo Mahakama ikahoji, iwapo hicho kilichosainiwa kilikuwa ni mkataba au la kwa mujibu wa sheria, ndipo wakaafikiana na hilo liwemo katika mambo yanayobishaniwa.

Awali, pande hizo zilikuwa zimeshindwa kukubaliana iwapo hoja hiyo inapaswa kuwa miongoni mwa viini vya kesi hiyo, ambavyo Mahakama inapaswa kuvizingatia katika uamuzi wake.

Baada ya kulitafakari suala hilo, Mahakama hiyo iliongeza kiini kingine cha sita ili iweze kuangalia endapo hicho kilichosainiwa ni mkataba kwa mujibu wa Sheria za Mikataba au vinginevyo. Kesi hiyo imefunguliwa na mawakili wanne kutoka mikoa tofauti, ambao ni Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus dhidi ya Serikali.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mshauri wa Serikali kwa masuala ya kisheria, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania, ambaye ni mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Bunge.

Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa jana kwa kuanza na pingamizi lililowasilishwa na Serikali, ikitaka mahakama hiyo isisikilize shauri hilo, badala yake ilitupilie mbali na kuandelea na usikilizwaji wa kesi ya msingi.

Hata hivyo, Serikali iliamua kuondoa pingamizi hilo ili kuruhusu usikilizwaji wa kesi ya msingi na kuamuriwa haraka.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mlwambo aliieleza mahakama kuwa wameamua kuondoa pingamizi hilo baada ya majadiliano na upande wa wadai. Amesema walifikia uamuzi huo baada ya kuangalia hoja na majibu ya pande zote.

"Na kwa kuzingatia kwamba hili ni shauri la kikatiba na kwamba ni vema umma wa Watanzania ukapata majibu kuhusu shauri hili, tumefikia uamuzi baada ya kukubaliana na waleta maombi, kwamba ili lisikilizwe kwa haraka tuondoe mapingamizi yote manne tuliyokuwa tumeyawasilisha hapa mahakamani," alisema Mlwambo.

"Na sababu kubwa kupisha usikilizwaji wa shauri mama na hakuna gharama kwa upande wowote," aliongeza na kisha akaiarifu Mahakama kuwa pia pande zote zimekubaliana mambo ambayo mahakama inapaswa kuyazingatia katika kutoa uamuzi.

Mmoja wa mawakili wa wadai, Mpale Mpoki aliieleza mahakama kuwa hawana pingamizi kuhusu hoja hiyo ya Serikali kuondoa pingamizi lake na kwamba wamejadiliana na wateja wao, nao wamekubaliana hivyo kwa kuwa wanalenga kuharakisha usikilizwaji na uamuzi wa kesi ya msingi.

Hivyo, Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote ilitoa amri ya kuondolewa kwa pingamizi hilo, amri ambayo ilitolewa na Jaji Dunstan Ndunguru, kiongozi wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, kwa niaba ya wenzake, Mustafa Ismail na Abdi Kagomba.

Mambo ya kuzingatia

Kisha Wakili Mpoki aliyataja mambo waliyokubakiana kuwa viini vya kesi hiyo kama ifuatavyo:

Mosi, kama kusaini, kuwasilisha bungeni na kuridhia mkataba wa Tanzania na Dubai kulikiuka kifungu cha 11 (1) na (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Rasilimali na Maliasili namba 5 ya mwaka 2017 na kifungu cha 5(1), 6(2) (a), (b), (e) na (i) cha Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba inayohusu Rasilimali na Maliasili za Nchi namba 6 ya mwaka 2017.

Mbili, kama umma uliarifiwa na kupewa muda muafaka kushiriki na kutoa maoni yao kama ambavyo sheria zinataka kuhusiana na utaratibu wa kupitisha na kuridhia mikataba.

Tatu, kama ibara ya 2(1), 4(2), 5(1), 6(2), 7(2), 8(1) (a-c), (2); 10(1) , 20(2) (a), (e) na (i) na (ii); 18, 21, 23(1) (3) na (4); 26, 27, na 30(2) za mkataba huo zinakiuka ibara za 1, 8, 28(1) na (3) za Katiba ya Tanzania.

Nne, kama ibara ya 2 na 23 ya mkataba huo zinakiuka kifungu cha 25 cha Sheria za Mikataba Tanzania. Tano, kama IGA (makubaliano) kati ya Tanzania na Dubai ilifuata taratibu za kisheria katika kuchagua njia ya manunuzi ambayo imewekwa chini ya kifungu cha 64 cha Sheria ya Manunuzi.

Baada ya kutaja mambo nayo, Wakili Mpoki alisema jambo ambalo halijakubaliwa ambalo limetolewa na upande mmoja (wadai) na upande mwingine haujalikubali ni kama wahusika katika mkataba unaobishaniwa walikuwa na nguvu ya kisheria kuingia kwenye mkataba.

Baada ya hoja hiyo, ndipo Jaji Mustafa alihoji kwa nini hawakukubaliana katika hilo (kama) ni moja ya kiini kinachopaswa kuamuriwa na Mahakama? Kisha akasema, kama kuna ubishani katika hilo, basi hicho pia kinapaswa kuwa kiini.

Akijibu swali hilo, Wakili wa Serikali, Stanley Kalokola alisema katika mambo waliyokubaliana wameangalia hoja zilizoletwa kwenye hati ya madai na wameona ni kweli hayo (matano) ndiyo yanayobishaniwa.

"Hoja kama walioingia kwenye mkataba walikuwa na nguvu za kisheria hatujaiona kwenye hati ya madai, lakini wenzetu wanasema ukisoma nyaraka zao ni kama wameiweka," alisema Kalokola.

Alisisitiza kuwa katika hilo, wao (mawakili wa Serikali) wanasema haipo na kuiweka jana ni kama kuwashtukiza, maana msingi wa mambo yanayolalamikiwa ni yale yanayoombwa kwenye hati ya madai. Hata hivyo, Wakili Mpoki alisema hoja hiyo inaonekana kwenye hati ya kiapo kinachounga mkono shauri hilo.

Alidai kuwa kesi hiyo si kama shauri la madai ya kawaida na kwamba katika shauri hilo taarifa zinapatikana kwenye kiapo na kwamba kwenye kiapo chao hoja hiyo ipo.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Kalokola alisisitiza kuwa bado ni msimamo wao kwamba hoja inayoibuliwa inatoka kwenye kiapo ambacho ni ushahidi na kwamba hoja zinazobishaniwa hazitoki kwenye kiapo, isipokuwa kwenye hati inayoanzisha madai.

"Ndiyo maana hata katika nafuu na amri wanazoziomba halipo hili," alisisitiza Wakili Kalokola, huku Mpoki naye akisisitiza kuwa hoja hizo zinawekwa kwenye kiapo.

Wakili Mpoki aliungwa mkono na mwenzake, Boniface Mwabukusi, aliyedai kuwa nyaraka zote, yaani hati ya madai na kiapo zinaambata na huwezi kuwasilisha hati ya madai peke yake bila kiapo.

Licha ya mabishano hayo, Jaji Ismail akirejea kiini cha nne kwamba ‘iwapo Ibara ya 2 na ya 23 za IGA zinakiuka kifungu cha 25 cha Sheria ya Mikataba’, alihoji kama hicho kilichosainiwa (IGA) ni mkataba kwa muktadha wa Sheria za mikataba.

Hivyo alipendekeza kuongeza kiini kimoja, yaani kama IGA (makubaliano hayo yaliyosainiwa) ni mkataba, hoja ambayo iliungwa mkono na mawakili wa pande zote, huku Wakili wa Serikali Mkuu, Edson Mweyunge akisema hoja hiyo itakuwa inahusisha pia na hoja waliyoshindwa kufikia muafaka, yaani kama waliosaini walikuwa na nguvu ya kisheria.

Kuongezeka kwa kiini hicho kilichopendekezwa na Mahakama, kulifanya jumla ya viini vya kesi vinavyobishaniwa kuwa sita badala ya vitano vya awali vilivyowasilishwa na mawakili wa pande zote.

Jaji Ndunguru alipendekeza kiini hicho kiwe cha nne ili kwenda na mtiririko mzuri.

Jaji Ndunguru aliahirisha kesi hiyo hadi leo itakapoanza kusikilizwa rasmi, hasa viini hivyo, ambapo wadai watatoa hoja zao na wadaiwa kutoa majibu. Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023, wanasheria hao wanapinga makubaliano hayo, wakidai ni batili kwa kuwa masharti ya baadhi ya ibara zake yanakiuka Sheria za Nchi za Ulinzi wa Rasilimali na Maliasili za Nchi na Katiba ya Nchi.

Vilevile wanadai kwamba yanahatarisha mamlaka ya nchi na usalama wa Taifa na kwamba yaliridhiwa na Bunge kinyume cha utaratibu bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao.

Makubaliano hayo yalisainiwa Oktoba 25, 2023 na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, baada ya kupewa nguvu ya kisheria na Rais Samia Suluhu Hassan, huku Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, akishuhudia na yaliridhiwa na Bunge Juni 10, 2023.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live