Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kutokamilika upelelezi kwakwamisha shauri la watumishi Tanesco

HUKUMU Kutokamilika upelelezi kwakwamisha shauri la watumishi Tanesco

Thu, 14 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kesi ya Uhujumu Uchumi namba 5/2023, inayomkabili Fundi Mchundo wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mwanza, Abdukadri Lwassa (39) na Ofisa Bohari wa Tanesco (mtunza stoo), Respicius Rwegoshora (33) imekwama kuendelea leo kutokana na upelelezi wake kutokamilika.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 125 likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya Sh2 bilioni huku wakidaiwa kutenda makosa hayo katika Ofisi za Bohari ya Tanesco iliyoko Nyakato jijini Mwanza kati ya Novemba 16, 2021 na Disemba 17, 2022.

Kesi hiyo iliitwa leo Septemba 13, 2023 kwa ajili ya kutajwa ambapo Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mwanahawa Changale ameiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa huku akidokeza kuwa upelelezi wake umekaribia kukamilika.

Kauli hiyo ya Changale, imepingwa vikali na jopo la mawakili wa utetezi katika shauri hilo akiwemo wakili wa mshtakiwa namba moja (Abdukadri Lwassa), Erick Mutta ambaye ameiomba mahakama kuihoji Jamhuri ili kupata uhakika wa lini upelelezi wa shauri hilo utakamilika.

Mutta amesema kuchelewa kwa upelelezi wa shauri hilo kunawafanya washtakiwa waendelee kusota rumande jambo ambalo amelitaja kama kuchelewesha haki ya wateja wao.

Kauli ya Mutta imeungwa mkono na mawakili wa mshtakiwa namba mbili (Respicius Rwegoshora), Amri Linus akisaidiana na Steven Kitale ambaye amesema tayari wameandika barua Mahakama Kuu kuomba amri ya wateja wao kupatiwa dhamana.

Wakili Linus amesema ombi lao limekubaliwa bila kuweka wazi masharti ya dhamana yaliyoainishwa katika majibu hayo huku akiomba shauri lipangwe kesho ili kukamilisha taratibu za dhamana kwa wateja wao kama ilivyoainishwa katika majibu ya barua hiyo.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela anayesikiliza shauri hilo, Fortunatus Kubaja baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi kesho Septemba 14, mwaka huu Saa 3:30 asubuhi, itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa kukamilisha masharti ya dhamana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live