Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kupewa dhamana mtuhumiwa, Polisi waingia matatani

42096 PIC+POLISI Kupewa dhamana mtuhumiwa, Polisi waingia matatani

Mon, 18 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Jeshi la polisi mkoani Mbeya limetupiwa lawama na familia ya mtoto yatima mwenye umri wa miaka 14 mkazi wa mtaa wa Itongo kata ya Mwakibete baada ya kumwachia kwa dhamana mtuhumiwa anayedaiwa kumfungia ndani na kumshambulia kwa kipigo Januai 31 mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi mjini hapa juzi, mlezi wa mtoto huyo, Ratifa Amos alisema kitendo cha kumwachia mtuhumiwa huyo kwa dhamana huku hali ya mtoto huyo ikiwa haijatengamaa kimeonyesha hakuna haki itakayotendeka kutokanana familia yao kuwa na maisha duni.

Alisema tangu Januari 31 mtoto huyo hajawahi kutumia chakula cha aina yoyote zaidi ya maji, chai, soda na dawa alizopatiwa na Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya alikokuwa akipata matibabu na hali yake haijatengamaa hivyo wanaomba haki itendeke.

Akizungumza kwa tabu mtoto huyo (jina linahifadhiwa) alisema siku ya tukio majira ya saa 2:00 usiku akiwa anawasha moto kwa ajili ya kumsaidia mama yake mlezi akitoka kazini afikie kupika chakula mtuhumiwa alimuita na kumtaka waende nyumbani kwake bila kumweleza sababu.

“Baada ya kufika alifunga mlango na kuanza kunishambulia kwa kipigo akinituhumu kumpatia binti yake (jina limehifadhiwa) Sh 200 kwa lengo la kumtaka kimapenzi jambo ambalo siyo kweli bali nilimpatia baada ya kuniomba,” alisema.

Balozi wa mtaa Itongo, David Mwaikambo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kitendo alichofanyiwa mtoto huyo ni cha kinyama akidai siku ya tukio mtuhumiwa alimfungia ndani na kumwadhibu kwa kipigo kwa saa zaidi ya tatu akimtuhumu kuhusika kimapenzi na binti yake.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Urlich Matei amekiri kutokea kwa tukio hilo na kushangazwa na kitendo cha polisi kumwachia mtuhumiwa kwa dhamana huku hali ya mtoto ikiwa haijatengamaa.

“Hata mimi kama mzazi sijafurahishwa na kitendo hiki, huyu kijana ameumizwa sana nimeona picha zake sijajua sababu ya mtuhumiwa kuachiwa kwa dhamana, hata hivyo tukio hili linaonekana kufichwa fichwa hili halitavumilika,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz