Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumekucha vita dawa za kulevya

Dawa Za Kulevya Mapambano (600 X 353) Kumekucha vita dawa za kulevya

Thu, 10 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema imeendelea kuhakikisha inadhibiti matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya, kwa lengo la kuwanusuru wananchi wake kuathirika na dawa hizo.

Akitoa taarifa leo mjini Dodoma ya mafanikio ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Balozi Pindi Chana, alisema jumla ya kilo 35, 227.5 zilikamatwa.

Alisema idadi hiyo ilijumuisha kilo 1124.52 za Heroin, gramu 811.3 za Cocaine, kilo 22,741.10 za bangi, kilo 10,931.72 za mirungi, gramu 4.92 za Morphine,na kilo 428.60 za methamphetamine.

“Kati ya dawa za kulevya zilizokamatwa, kilo 859.36 zilikamatwa siku moja kwa watuhumiwa saba raia wa Iran na kuvunja rekodi kuwa ni ukamataji wa kwanza wa kilo nyingi zilizokamatwa kwa pamoja tangu nchi yetu ipate uhuru,” amesema.

Pia alieleza kuwa ekari 185 za mashamba ya bangi na ekari 10 za Mirungi ziliteketezwa mkoani Pwani katika Wilaya ya Rufiji.

Mbali na hayo, jitihada zingine zinazofaywa na Serikali ni pamoja na kutoa huduma ya matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya, ambapo kliniki sita za tiba ya Methadone zimeanzishwa katika maeneo ya Songwe katika maeneo mbalimbali nchini.

Uanzishwaji wa kliniki hizo kunafanya jumla ya kliniki 15 kuwepo nchini, zikihudumia zaidi ya waathirika 10,600 wa dawa za kulevya kila siku.

Pia serikali imekuwa ikisimamia upatikanaji wa uhakika wa dawa ya methadone kwa ajili ya tiba ya waraibu wa heroin kwa kusimamia uagizaji, usambazaji na udhibiti wake.

“Vijana 200 wanaopatiwa matibabu kwenye kliniki za Methadone wamejumuishwa katika programu ya kukuza ujuzi kupitia vyuo vya VETA, ili kuwajengea ujuzi wa kufanya kazi za kiuchumi na kuachana na dawa za kulevya,” alisema.

Pia amesema zimeanzishwa klabu za kupinga dawa za kulevya shuleni na elimu imetolewa kwa walimu 66, ili kuwawezesha kusimamia klabu hizo.

Alifafanua kuwa elimu juu ya tatizo la matumizi na biashara ya dawa za kulevya iliwafikia wanachuo 1,700 katika vyuo mbalimbali nchini.

Pia alisema elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya, imekuwa ikitolewa kupitia vyombo vya habari, warsha za kitaifa, mbio za Mwenge, makongamano na mitandao ya kijamii.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live